Wednesday, October 18, 2017

MANISPAA SONGEA YATOA MILIONI 49 KUWEZESHA WAJASIRIAMALI WAKE

Kutoka kulia aliyesimama ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini, Leonidas Gama akisisitiza jambo juu ya namna ya kuwajali na kuthamini vikundi vya wajasiriamali vya vijana na wanawake na upande wa kushoto aliyeketi ni Meya wa Manispaa ya Songea Abdul Mshaweji.
Na Mwandishi wetu,        
Songea.

IMEELEZWA kuwa Wajasiriamali wadogo wadogo waliopo katika halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, watanufaika na mkopo wa shilingi milioni 49 ambao umetolewa na halmashauri hiyo, kwa ajili ya kuwawezesha wasonge mbele kimaendeleo katika shughuli zao za ujasiriamali.

Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa hiyo, Naftari Saiyoloi alitoa taarifa hiyo juzi mjini hapa, katika uzinduzi wa mfuko wa vijana na wanawake.

Saiyoloi alibainisha kuwa shilingi milioni tisa zitakopeshwa kwa vikundi kumi vya vijana na shilingi milioni 40 zitakopeshwa vikundi 39 vya wanawake.


Pia alisema kuwa kuanzia mwaka wa fedha wa 2014/2015 hadi 2017/2018 Manispaa ya Songea imeweza kuwapatia zaidi ya shilingi milioni 181 mfuko wa wanawake na vijana katika vikundi vyao waweze kufanya shughuli zao za maendeleo.

Kati ya fedha hizo shilingi milioni 116 zinatokana na mapato ya ndani na zaidi ya milioni 65 zinatokana na marejesho yaliyofanyika kutokana na vikundi hivyo vinavyokopeshwa kurejesha mkopo husika.

“Idadi ya vikundi vya wanawake vilivyonufaika kwa fedha hizi ni 202 na kiasi kilichokopeshwa ni zaidi ya milioni 126, idadi ya vikundi 115 vya vijana vilinufaika pia na mkopo wa zaidi ya milioni 55”, alisema Saiyoloi.

Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo huyo aliongeza kuwa Manispaa katika kipindi hicho ilitoa jumla ya shilingi milioni 92 kutoka kwenye mapato yake ya ndani kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana.

Alisema kati ya fedha hizo shilingi milioni 3.2 zilitumika kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji na milioni 88.8 vilikopeshwa vikundi vya wanawake 77 kiasi cha shilingi milioni 59.8 na vikundi vya vijana 56 vilikopeshwa milioni 29.

Alisisitiza kuwa fedha za vikundi vya wanawake zilizorejeshwa ni zaidi ya shilingi milioni 53 na fedha za vikundi vya vijana zilizorejeshwa ni zaidi ya shilingi milioni tisa.

Mgeni rasmi katika utoaji wa mikopo hiyo ambaye alikuwa ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini, Leonidas Gama alipongeza jitihada hizo zinazofanywa na Manispaa ya Songea kwa kutoa kwa wakati asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kwenda kukopesha vijana na wanawake.


Hata hivyo Gama alisema mikopo hiyo ni muhimu kwa wanawake na vijana kwa sababu umaskini mkubwa upo katika ngazi ya familia, hivyo itaweza kupunguza makali ya maisha na hatimaye hata umaskini kupungua kwa wale waliokuwa wanyonge.

No comments: