Monday, October 30, 2017

WASIMAMIZI MTIHANI KIDATO CHA NNE WAPEWA ONYO KALI

Katibu Mtendaji wa Baraza la mitihani Tanzania, Dokta Charles Msonde.
Na Mwandishi wetu,

WAKATI Watahiniwa 385,938 wanatarajiwa kuanza mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka huu leo, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limetoa onyo kali kwa wasimamizi wa mtihani huo.

Baraza hilo limesema kuwa halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wasimamizi hao wa mitihani, pale itakapobainika kuna udanganyifu wa aina yoyote ile.

Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dokta Charles Msonde alitoa onyo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema watahiniwa wa shule watakuwa 323,513 na wa kujitegemea 62,425.


Dokta Msonde alisisitiza kwa kuwataka wasimamizi wa mtihani huo kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwa kuwa yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua.

Alisema kuwa hivi sasa udanganyifu umepungua, na kwamba mwaka 2011 watahiniwa waliofutiwa mitihani walikuwa ni 9,739 na mwaka jana walikuwa 500 kutokana na vitendo hivyo vya udanganyifu.

Pia aliongea kuwa watahiniwa hao walibainika kufanya udanganyifu kwa kuingia na simu, vitabu na notisi kwenye vyumba vya mitihani.

Dokta Msonde pia aliwakumbusha wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mitihani hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha mitihani.

“Baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litajiridhisha kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa mitihani ya taifa”, alisisitiza.

Alisema mitihani ya kidato cha nne na maarifa (QT) itafanyika kwa siku 19 kuanzia leo na utahusisha jumla ya shule za sekondari 4,787 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 1,064.

Alibainisha kuwa kati ya watahiniwa wa shule 323,513 waliosajiliwa, wavulana ni 159,103 sawa na asilimia 49.18 na wasichana ni 164,410 sawa na asilimia 50.82.

Kadhalika alieleza kuwa watahiniwa 58 ni wale wasioona na watahiniwa wenye uono hafifu ni 305 ambao maandishi ya karatasi zao za mitihani hukuzwa. Mwaka jana idadi ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa ni 355,822.

Dokta Msonde alisema kati ya watahiniwa wa kujitegemea 62,425 waliosajiliwa, wavulana ni 28,574 sawa na asilimia 45.77 na wasichana ni 33,851 sawa na asilimia 54.23.

Alisema watahiniwa wa kujitegemea wasioona ni sita, kati yao wasichana ni watano na kwamba mwaka jana idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa ilikuwa ni 52,550.

Alisema jumla ya watahiniwa 16,279 wamesajiliwa kufanya mtihani wa maarifa (QT) kati yao, wanaume ni 6,725 sawa na asilimia 41.31 na wanawake ni 9,554 sawa na asilimia 58.69 wakati mwaka jana idadi yao ilikuwa ni 20,655.

Pia katika eneo la shule Dokta Msonde alitoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha kwamba mitihani hiyo inafanyika kwa amani na utulivu.

“Wananchi na waandishi wa habari wanaombwa kuheshimu eneo la mitihani, hairuhusiwi mtu yeyote asiyehusika na mitihani hii kuingia kwenye eneo la shule katika kipindi chote cha mitihani, hizi ni taratibu zilizowekwa naomba ziheshimiwe”, alisema.

Amewataka watahiniwa wote wakumbuke kwamba mtihani wa kidato cha nne ni muhimu kwa sababu unawapima uwezo na uelewa wao na matokeo ya mtihani huu hutumika katika uchaguzi wa kujiunga na kidato cha tano pamoja na fani mbalimbali za utaalamu wa kazi.

Alizitaka kamati za mitihani za mikoa na halmashauri kuhakikisha taratibu zote za uendeshaji wa mitihani zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usalama na utulivu wa vituo vya kufanyia mitihani.


“Tumaanini walimu wamewaandaa vizuri wanafunzi katika kipindi chote cha elimu yao ya sekondari, ni matarajio ya baraza kuwa wanafunzi watafanya mitihani yao vizuri kwa kuzingatia kanuni za mitihani”, alisema Dokta Msonde.

No comments: