Wednesday, October 25, 2017

WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA KUWABANA MAFISADI

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

WANANCHI wa kijiji cha Lukalasi kitongoji cha Ngembambili kijiji cha Mkako wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli kwa kazi anayoendelea kuifanya ya kuwaibua mafisadi na kuwachukulia hatua wakiwemo wezi wa madini.

Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na wachimbaji wadogo wa madini ambao wanaishi katika maeneo hayo mbele ya mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na Mkuu wa mkoa huo, Dokta Binilith Mahenge.

Masha Mussa na Silvano Challe wakazi wa Ngembambili kwa nyakati tofauti walisema kuwa kitendo anachokifanya Magufuli na kuwabana mafisadi hao ambao walikuwa wanadhoofisha uchumi wa nchi, ni ujasiri wa hali ya juu hivyo wamemwomba aendelee kukaza kamba zaidi ili kuweza kudhibiti vitendo hivyo viovu visiweze kuendelea kutokea.


Aidha Challe alimwomba Mkuu huyo wa mkoa kuwabana wachimbaji wadogo wa madini wa eneo hilo la Ngembambili ambao wanakwepa kulipa kodi ya Serikali na ikiwezekana wachukuliwe hatua haraka iwezekanavyo jambo ambalo lilimlazimu mmiliki wa eneo la kuchimba madini aina ya Vito, Sighe Mahundi kukiri mbele ya Dokta Mahenge kuwa kwa muda wa miaka miwili sasa alikuwa hajalipia leseni ya kuchimba madini katika eneo hilo.

Pia alisema kuwa wanaiomba Serikali kuona umuhimu wa kuwaletea umeme kwenye kijiji hicho, ambao utaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika ufanyaji wa kazi zao kwani kijiji hicho kuna mgodi wa uchimbaji wa dhahabu, taasisi mbalimbali pamoja na wananchi ambao wanahitaji huduma hiyo ya umeme.

“tunaipongeza Serikali kwa kuweka pia miundombinu mizuri ya barabara ya kutoka Mkako hadi hapa Lukalasi hivyo tunaomba mradi wa Umeme Vijijini (REA) kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi wa Lukalasi”, alisema.

Mmiliki wa mgodi wa dhahabu uliopo lukalasi Johnson Nchimbi alimweleza Mkuu wa mkoa, Dokta Mahenge kuwa kwa muda mrefu mgodi wake umekuwa ukifanya kazi chini ya kiwango kwa sababu kunatatizo kubwa la umeme kwani wamekuwa wakitumia umeme wa jenereta hivyo endapo umeme wa REA utawafikia wataweza kuongeza uzalishaji mkubwa wa madini hayo na ameiomba Serikali kutekeleza hilo ili waweze kuondokana na adha kubwa wanayoipata hivi sasa.

Kwa upande wake Dokta Mahenge alitoa muda wa siku mbili kwa wachimbaji hao wa madini ambao walikuwa hawalipi leseni walipe kwa kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali huku akimwagiza Kamishna msaidizi wa madini Kanda ya ziwa Nyasa, Mhandisi Mahobe kuhakikisha kwamba ofisi yake inasimamia kikamilifu suala hilo ili Serikali iweze kupata mapato yake.


Alisema kuwa mkoa wa Ruvuma unahazina kubwa ya madini ya dhahabu, shaba, chuma, vito, madini ya viwandani, mawe, kokoto, nishati na urenium huku akiwaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mkoa huo kuona umuhimu wa kusimamia kikamilifu rasilimali hizo zilizopo kwenye maeneo yao kwa lengo la kudhibiti pia wanaokwepa kulipia leseni zao za uchimbaji.

No comments: