Thursday, October 12, 2017

WANANCHI MITENDEWAWA NA CHANDARUA SONGEA KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI SAFI NA SALAMA

Mhandisi wa maji Manispaa ya Songea, Samwel Sanya aliyesimama katikati akitoa maelezo mafupi juu ya maendeleo ujenzi mradi wa maji safi na salama katika mtaa wa Mitendewawa na Chandarua katika Manispaa hiyo kwa Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema aliyesimama upande wa kushoto ambaye amevaa suti rangi nyeusi.
Na Albano Midelo,
Songea.

MTAA wa Mitendewawa na Chandarua iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wananchi wake wanatarajia kunufaika na kuondokana na adha ya upatikanaji wa maji safi na salama, baada ya serikali kuanza kujenga mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 517.

Samwel Sanya ambaye ni Mhandisi wa Maji katika Manispaa hiyo alisema hayo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema wakati Mkuu huyo wa wilaya alipofanya ziara yake ya ukaguzi wa mradi huo.

Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ulitakiwa kuanza mwaka wa fedha wa 2014/2015 lakini utekelezaji wake haukufanikiwa kutokana na fedha hizo kuchelewa kuwafikia kutoka Serikali kuu.


Mhandisi Sanya alisema utekelezaji wa mradi huo ambao una urefu wa kilometa 13.4 ukiwa na vituo 13 vya maji, umeanza katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 ambapo Mkandarasi husika amefikia zaidi ya asilimia 60 ya utekelezaji huo.

Alifafanua kuwa kisima cha mradi huo kina urefu meta 68 na kwamba uwezo wake ni kuzalisha maji lita 7,000 kwa saa moja ambapo wanufaika wa mradi watakuwa wakazi zaidi ya 840 katika mitaa hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Songea mara baada ya kuukagua alimtaka Mhandisi huyo kuhakikisha kwamba mradi unajengwa kwa ubora unaotakiwa na kumaliza ujenzi kwa wakati uliopangwa.


Mkoa wa Ruvuma unakadiriwa kuwa na wakazi 1,497,853 kati ya hao ni wakazi 851,034 sawa na asilimia 57 tu ndiyo wanaopata maji safi na salama, kwa mujibu wa takwimu za hadi kufikia Oktoba mwaka jana.

No comments: