Sunday, October 15, 2017

WATU 2,458 MANISPAA SONGEA HAWAJUI KUSOMA NA KUANDIKA

Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema akikagua zana za kufundishia katika Manispaa ya Songea.
Na Albano Midelo,
Songea.

IMEELEZWA kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, ina Watu Wazima 2,458 ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

Afisa elimu ya Watu Wazima, Faraja Yonas alisema hayo juzi ambapo alifafanua kuwa kati yao wanaume ni 661 na wanawake ni 1,797.

Yonas alibainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za usajili mwezi Januari hadi Machi mwaka huu, Manispaa hiyo ina jumla ya Watu Wazima 119,328 ambapo kati yao wanaume ni 58,049 na wanawake ni 61,279.


Alisema kuwa hivi sasa Manispaa ya Songea imejipanga vizuri katika harakati za kuhakikisha kwamba watu wazima wote wanajua kusoma, kuhesabu na kuandika Kwa asilimia 100.

Anaitaja mikakati ambayo Manispaa inachukua kutekeleza lengo hilo la Elimu ya Watu Wazima kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa Watu Wazima kwa kuwapatia stadi za kazi muhimu kwa ajili ya kuboresha mipango ya maendeleo katika sekta hiyo.

Mikakati mingine ni kuongeza ujuzi wa uzalishaji mali na kuyafahamu mazingira yao kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kuweza kuyakabili vyema mazingira yao na kufikia lengo kuu la Elimu ya Watu Wazima.

Akizungumzia kuhusiana na kisomo chenye manufaa na  kisomo cha kujiendeleza na uzalishaji mali katika Manispaa hiyo, Yonas alisema Manispaa ina vituo 108 vya MUKEJA vyenye washiriki 2,600, wakiwemo wanaume 937 na wanawake 1,663.

MUKEJA ni Mpango wa uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii hivyo katika mpango huu washiriki hujifunza mambo yanayohusu uchumi na maendeleo ya jamii kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kusoma, kuandika na kuhesabu.

Katika mfumo huo washiriki wenyewe ndiyo wanaopanga jambo la kujifunza, muda muafaka wa kujifunza na namna ya kujifunza na kwamba Mukeja ni mtaala unaozingatia matakwa ya mwanakisomo katika kujifunza.

Afisa elimu huyo aliongeza kuwa Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Waliokosa (MEMKWA) alifafanua kuwa mpango huo unalenga kuwapatia elimu watoto walioikosa elimu ya msingi, ambao wengi wao wanatoka katika mazingira magumu au familia zenye kipato duni.

Manispaa ya Songea ina vituo tisa vya MEMKWA, vyenye jumla ya wanafunzi 103 kati yao wavulana 50 na wasichana 53.


Pia kulingana na maelezo ya Afisa Elimu ya Watu Wazima alisema Manispaa hiyo ina jumla ya wana kisomo 154 ambapo wanahudhuria masomo, ambapo hivi sasa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Cuba zina mpango wa kutoa Elimu ya Watu Wazima kwa kutumia Redio, Video na Televisheni.

No comments: