Tuesday, October 24, 2017

TFDA MANISPAA SONGEA YAKAMATA DAWA AMBAZO HAZIFAI KWA MATUMIZI YA BINADAMU

Mratibu wa Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) katika Manispaa ya Songea, Vitalis Mkomela akionesha dawa za aina mbalimbali kwa waandishi wa habari ambazo zimepita muda wake wa matumizi. 
Na Albano Midelo,
Songea.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) katika Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma, imekamata dawa za binadamu ambazo zilikuwa zinaendelea kuuzwa zikiwa zimepita muda wake katika baadhi ya maduka ya dawa muhimu yaliyopo mjini hapa.

Mratibu wa TFDA katika Manispaa hiyo, Vitalis Mkomela alisema kuwa dawa za aina mbalimbali zenye thamani ya shilingi 244,000 zilikamatwa katika operesheni maalum ambayo ilifanywa na watalaamu wa idara ya afya.

Mmiliki wa duka moja ambalo lilikutwa na dawa hizo amekiri kuuza dawa hizo zilizomalizika muda wake na kwamba tayari amepigwa faini ya shilingi 600,000.


Mamlaka hiyo inatoa rai kwa wananchi wa Manispaa ya Songea wanaponunua dawa kusoma kwanza maelekezo, yakiwemo yale ambayo yanaonesha dawa zilitengenezwa mwaka gani na tarehe ya mwisho wa matumizi.

Mkomela alisema kuwa raia mmoja ambaye alikwenda kununua dawa na kubaini aliuziwa dawa ambazo muda wake umepita ndipo aliweza kuisaidia TFDA kufanya ufuatiliaji na kuweza kufanikiwa kukamata dawa hizo ambazo zinaweza kuleta madhara makubwa kwa binadamu.

Alisisitiza kuwa TFDA itaendelea kufanya operesheni za kushitukiza na kukagua maduka ya dawa na vipodozi katika Manispaa ya Songea hiyo.

Katika Manispaa ya Songea pia TFDA imekamata diapers (Nepi) ambazo muda wake umemalizika tangu Agosti mwaka huu zikiendelea kuuzwa katika baadhi ya maduka yaliyopo Soko kuu la Songea mjini.


Mratibu huyo wa TFDA katika Manispaa hiyo alisema wamekamata Nepi aina ya Ponpon 65 zenye thamani ya shilingi 277,500 ambapo mmiliki husika naye alikiri kuuza bidhaa hizo ambazo muda wake umepita hivyo alipigwa faini ya shilingi zaidi ya lakini moja ikiwemo na gharama za kuteketeza mzigo huo.

No comments: