Friday, October 13, 2017

MANISPAA SONGEA YAVUNJA MKATABA NA MKANDARASI

Hii ni moja kati ya sehemu ya barabara mtaa wa FFU kwenda Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami nzito katika Manispaa ya Songea.
Na Mwandishi wetu,     
Songea

HATIMAYE Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imevunja rasmi Mkataba ujenzi wa lami nzito kati yake na Kampuni ya Lukolo yenye makao makuu yake Jijini Dar es salaam.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Mhandisi Samwel Sanya alisema kuwa wamechukua maamuzi hayo baada ya muda wa Mkataba wa kumaliza kazi kwa Mkandarasi huyo ulimalizika tangu Juni 30 mwaka huu.

Alisema kuwa baada ya muda huo kumalizika Mkandarasi huyo aliingizwa kwenye tozo (Liquidated Damage) na kwamba iwapo atashindwa kumaliza kazi kwa siku 100 hatua za kisheria za kuvunja mkataba zitafanyika.


“Oktoba 8 mwaka huu ndiyo siku 100 alizopewa Mkandarasi huyo zimemalizika hivyo tumevunja mkataba rasmi na Mkandarasi huyu, amekatwa asilimia 10 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 1.4 kwa kuchelewesha mradi na anatakiwa kulipa asilimia 15 ya fedha kwa kazi ambazo hajamaliza ndani ya mkataba”, alisema Sanya.

Mkandarasi huyo pia anatakiwa kurudisha kiasi cha fedha shilingi bilioni 2.15 ambazo zilitolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) fedha ambazo zilitolewa kwa ajili ya kufanya kazi ya kusafirishia mitambo mbalimbali ya ujenzi katika mradi huo.

Kaimu Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Songea alifafanua kuwa baada ya kuvunjwa mkataba huo, Manispaa itaanza mchakato wa kumtafuta Mkandarasi mwingine ili aweze kuendelea na kazi zilizobaki katika ujenzi wa barabara hiyo.

Zaidi ya shilingi bilioni 14 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara za mji wa Songea katika kiwango cha lami nzito zenye urefu wa kilometa 8.6.

Fedha za mradi huo zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo Serikali za mitaa (ULGSP), ambapo mpango huo unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za Miji na Manispaa 18 za Tanzania bara ikiwemo Manispaa hiyo.

Mradi huo ambao ulianza kujengwa Juni Mosi mwaka 2015 ulitarajiwa kukamilika Juni 30 mwaka huu ambapo fedha iliyopokelewa na Manispaa ni  zaidi ya shilingi bilioni saba ambapo hadi sasa Mkandarasi huyo alikwisha lipwa zaidi ya shilingi bilioni nne.

Barabara za Manispaa ya Songea ambazo zipo kwenye mradi huo ni katika mtaa wa FFU hadi Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2, barabara ya shule ya sekondari ya wasichana Songea hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5 na barabara ya Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.


Vilevile barabara nyingine ni Mitumbani hadi Yapenda yenye urefu wa kilometa moja, barabara ya Polisi hadi Stendi ya Mlilayoyo yenye urefu wa kilometa 0.45.

No comments: