Thursday, October 12, 2017

MWANSASU MWENYEKITI MPYA WA CHAMA CHA MAPINDUZI NAMTUMBO

Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma wamemchagua, Aggrey Mwansasu kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM wilayani humo baada ya kumbwaga chini aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Benjamini Nindi.

Uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti huyo ulifanyika juzi kwenye ukumbi wa shule ya Sekondari Namtumbo, ambayo inamilikiwa na Jumuiya ya wazazi ya Chama Cha Mapinduzi iliyopo mjini hapa.

Katika uchaguzi huo awali uliingia dosari baada ya msimamizi wa uchaguzi huo, Zena Mijinga kujisahau kwa kutosoma kanuni ya ushindi wa uchaguzi huo ambapo mgombea ni sharti apate kura zaidi ya nusu ya wapiga kura waliopo kwenye uchaguzi huo.


Kutosomwa kwa kanuni hiyo na wagombea hao wa nafasi hiyo kutofikia nusu ya kura zilizopigwa iliwataka wajumbe wa mkutano huo kurudia kupiga kura kwa nafasi hiyo ya Mwenyekiti, jambo ambalo liliibua hasira kutoka kwa wajumbe wakidai kwamba hali hiyo inaonesha kutaka kumbeba mgombea mmojawapo katika uchaguzi huo huku wakiongeza kuwa kanuni hiyo kwa nini haikusomwa kabla ya uchaguzi.

Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo, Fadhil Kitete alionekana kuokoa jahazi kutoka kwa baadhi ya wajumbe waliotaka kukataa kurudia kwa uchaguzi huo huku akiwaomba wajumbe hao radhi kwa kutosoma kanuni hiyo kabla ya uchaguzi na kusema kuwa ni kosa la kibinadamu limefanyika na kwamba aliwataka wajumbe waridhie kurudia kupiga kura kwa nafasi hiyo ya Mwenyekiti kwa kuzingatia kanuni hiyo.

Kitete aliongeza kuwa kanuni ndiyo siku zote inayoongoza uchaguzi na kurudia uchaguzi ambapo haitazuia wajumbe kumchagua mgombea wanayemtaka.

Baadaye wajumbe kwa pamoja walikubaliana na hoja hiyo na hatimaye kuweza kupiga kura na kumchagua Mwenyekiti wa CCM wilayani humo ambaye walimtaka.

Waliogombea  nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Namtumbo walikuwa wanne ambao ni Legani Luambano, Yordani Fusi, Benjamini Nindi  na Aggrey Mwansasu ambapo katika uchaguzi wa awali Legani Luambano alipata kura 20, Yordani Fusi alipata kura 25, Benjamini Nindi aliyekuwa akitetea kiti hicho alipata kura  290 na Aggrey Mwansasu alipata kura 304 kati ya kura  645 zilizopigwa.

Uchaguzi  wa marudio uliwashindanisha  wagombea wawili Benjamini Nindi  na Aggrey Mwansasu ambao walionesha kuwa na ushindani mkubwa kwa wajumbe, lakini mpaka mwisho wa uchaguzi huo msimamizi wa uchaguzi huo  Zena Mijinga alimtangaza  Aggrey  Mwansasu kuwa mshindi  kwa nafasi  ya Mwenyekiti kwa kumbwaga mpinzani wake Benjamini Nindi  aliyekuwa anatetea  nafasi hiyo.

Mijinga alimtangaza  Aggrey Mwansau  kuwa ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 369 dhidi ya  kura 228 alizopata  mpinzani wake  kati ya kura 610 zilizopigwa ambapo kura 13 ziliharibika  katika  uchaguzi huo.


Hata hivyo katika mkutano huo pia walichaguliwa wajumbe  wawakilishi wa mkutano mkuu wa Taifa, mkutano mkuu wa mkoa  na  viongozi wa nafasi ya katibu wa siasa itikadi na uenezi, jumuiya  ya wanawake, vijana na wazazi.

No comments: