Sunday, October 22, 2017

SERIKALI YAPONGEZWA KWA KUBORESHA ELIMU KATIKA SHULE ZA MSINGI, SEKONDARI NA VYUO VIKUU

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

MJUMBE wa Kamati tendaji Taifa ya Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Ruvuma, Sabina Lipukila ameipongeza Serikali ya awamu ya tano ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dokta John Pombe Magufuli kwa kuona umuhimu wa kuboresha shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu hapa nchini ikiwa ni lengo la kuhakikisha vijana wote wanapata elimu bora.

Hayo yalisemwa juzi na Mjumbe huyo katika mahafali ya tatu ya kuhitimu wanafunzi wa kidato cha nne, katika sekondari ya kutwa ya Mahanje iliyopo Madaba wilayani Songea mkoani hapa.

Alisema kuwa kufuatia hali hiyo wananchi wanapaswa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini ili watoto wanaosoma katika shule hizo waweze kuwa katika mazingira mazuri.


Katika mahafali hiyo, Lipukila alichukua pia jukumu la kuendesha harambee kwa watu waliohudhuria sherehe hizo ili ziweze kutatua changamoto zilizopo katika shule hiyo ambapo zaidi ya shilingi milioni 3,000,000 ziliweza kupatikana baada ya wadau mbalimbali kuweza kuchangia.

Mapema Mkuu wa shule ya sekondari Mahanje, Lucynes Mbuba alisema kuwa shule yake ilianzishwa mwaka 2012 na iliendelea kujengwa na vijiji viwili vya Madaba na Mahanje ambapo hadi sasa shule hiyo inawanfunzi 247 kati yao wavulana 130 na wasichana 117.

Alieleza kuwa jumla ya wanafunzi 43 ndio wanaotarajiwa kuhitimu elimu ya sekondari ya kidato cha nne kati yao wavulana ni 20 na wasichana 23 hivyo wanafunzi 24 wameshindwa kuhitimu kidato cha nne kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro wa kudumu, kupata mimba, umaskini uliokithiri katika jamiina wengine kuhama kutokana na uhaba wa miundombinu iliyopo hapo shuleni.

Mbuba alifafanua kuwa kwa kuzingatia falsafa ya elimu ya kujitegemea shughuli mbalimbali zinafanywa na shule hiyo ambazo ni kilimo cha mboga mboga (bustani), kilimo cha migomba na viazi ambapo kimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuwajengea wanafunzi ari ya kupenda kufanya kazi.

Amezitaja changamoto zinazoikabili shule yake kuwa ni ukosefu wa mashine ya kudurufu mitihani ambapo hulazimika kuwapima wanafunzi wao kwa kuandika majaribio ubaoni matokeo yake ya upimaji huo huwa ni ya kiwango cha chini.

Vilevile shule inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa bwalo la chakula ambapo wanafunzi hupata adha kubwa hasa kipindi cha masika pale unapofikia muda wa kula chakula kutokana na kukosa sehemu ya kukaa wanapokula chakula.


Changamoto nyingine ni uhaba wa nyumba za walimu, vyumba vya maabara havijakamilika ujenzi wake, kuna tatizo la mfumo wa gesi na mfumo wa maji pia kuna tatizo la ukosefu wa maktaba na upungufu wa samani za ofisi za walimu hivyo wanaiomba Serikali na wadau mbalimbali kuona umuhimu wa kusaidia uwezekano wa kupunguza changamoto zinazoikabili shule hiyo.

No comments: