Friday, October 6, 2017

MILIONI 127 KUTUMIKA UJENZI WA DARAJA MATARAWE SONGEA

Upande wa kushoto, Mkuu wa wilaya ya Songea Palolet Mgema akitoa msisitizo juu ya ujenzi wa daraja la Matarawe alipofanya ziara yake juzi.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, Palolet Kamando Mgema amefanya ziara ya kushitukiza kukagua ujenzi wa daraja la mto Matarawe lililopo katika Manispaa ya Songea mkoani humo.

Ziara hiyo imefanyika juzi ambapo daraja hilo limekuwa ni kiungo muhimu kwa wananchi wa Kata ya Matarawe, Mjimwema na kata nyingine jirani mjini hapa.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Injinia Samwel Sanya alisema kuwa zaidi ya shilingi milioni 127 zimetengwa kwa ajili ya kazi ya kukamilisha ujenzi wa daraja hilo.


Mradi huo kazi zake zitakazofanyika zitakamilika kwa muda wa miezi sita ambapo ulianza Juni mwaka huu na unatarajia kukamilika ifikapo Disemba 2017.

Ubovu wa daraja hilo umekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Manispaa ya Songea hali ambayo imekuwa ikisababisha hata ajali za mara kwa mara ikiwemo hasa kipindi cha masika.

Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea kumsimamia Mkandarasi husika ili  aongeze kasi ya ujenzi wa daraja hilo, na mradi uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa ili wananchi waweze kuanza kulitumia daraja hilo ambalo ni kiungo muhimu kwa mawasiliano yao.


Licha ya kukagua daraja hilo, Mkuu huyo wa wilaya alitembelea pia na kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi katika Manispaa hiyo na kutoa maagizo ya kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo kwa wakati ili jamii iweze kunufaika nayo.

No comments: