Wednesday, October 4, 2017

VITUO VYA ELIMU VISIVYOSAJILIWA SONGEA MARUFUKU KUTOA HUDUMA

Ofisi za Halmashauri Manispaa ya Songea.
Na Albano Midelo,
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani hapa, imewaandikia barua wamiliki wote wa vituo vya kutolea elimu yoyote bila kusajiliwa kuacha mara moja tabia hiyo, kwa kuwa ni kinyume cha sheria za nchi na endapo kutakuwa na mtu anafanya hivyo atachukuliwa hatua kali ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Idara ya elimu katika Manispaa hiyo imetoa agizo hilo juzi kwa Waratibu elimu kata wote waliopo kwenye Manispaa ya Songea kusimamia ipasavyo utekelezaji wake ambapo kuanzia mwezi uliopita Septemba mwaka huu imepigwa marufuku hairuhusiwi mmiliki wa shule au kituo chochote kile cha kutolea mafunzo ya tuition kutoa masomo bila kusajiliwa.

Imebainisha kuwa kumeibuka taasisi zisizokuwa rasmi na watu binafsi kuanzisha vituo vya elimu na kujitangaza kwa njia mbalimbali kwamba wanatoa masomo ya ngazi mbalimbali ya elimu kuanzia elimu ya chekechea, msingi, sekondari na vyuo.


Kitendo cha kuanzisha vituo hivyo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu husika kwa sababu kuanzisha shule au kituo kuna taratibu zake ikiwemo kupata usajili wa kisheria na kufuata taratibu nyingine zinazotolewa mara tu baada ya kupata usajili huo.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia hutoa taratibu na miongozo ya kufungua na kuendesha shule, vyuo na vituo vya elimu vya umma na watu binafsi kwa ajili ya kutoa elimu rasmi na isiyokuwa rasmi kwa wananchi.


Kwa watu ambao wanataka ufafanuzi zaidi wanapaswa kuwasiliana na Idara ya elimu Manispaa ya Songea au kupitia kitengo chake cha Elimu ya watu wazima ambao ndiyo wanatoa utaratibu wa jambo hili.

No comments: