Friday, October 27, 2017

BREAKING NEWS: KIKAO BARAZA LA MADIWANI MJI WA MBINGA CHAVUNJIKA MKURUGENZI MTENDAJI AKALIA KUTI KAVU AJIKUTA AKIWA KATIKA WAKATI MGUMU

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga leo wakiwa wamekusanyika nje ya ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa wa kufanyia kikao chao cha baraza la Madiwani, kabla ya kikao hicho cha baraza kuanza kufanyika.

Aliyesimama ni Diwani wa kata ya Mpepai halmashauri ya mji wa Mbinga, Benedict Ngwenya akichangia hoja ya kukataa kuendelea na kikao cha baraza la Madiwani wa mji huo, wakitaka mpaka Mkurugenzi mtendaji Robert Kadaso Mageni atoke nje ya kikao ndipo waendelee na kikao ambapo hata hivyo kikao hicho kilivunjika hawakuweza kuendelea nacho. 

Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga na baadhi ya waalikwa wakitoka nje ya ukumbi baada ya kikao cha baraza la Madiwani hao kuvunjika.
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, kimeshindwa kufanyika na badala yake kimevunjika kufuatia Madiwani hao kumkataa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Robert Kadaso Mageni wakidai kuwa hawataki kufanya naye kazi tena kutokana na Mkurugenzi huyo kushindwa kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo ya wananchi wa halmashauri hiyo.

Madiwani hao walichukua maamuzi hayo magumu leo katika kikao hicho ambacho walitakiwa kupokea taarifa za maendeleo ya wananchi, robo ya kwanza ya mwaka kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

Aidha maamuzi hayo yalifikiwa baada ya Mwenyekiti wa Madiwani hao, Kipwele Ndunguru kufungua kikao cha baraza hilo na kuwataka Madiwake wake wapokee agenda za kikao, ambapo kwa pamoja walimkatalia kupokea agenda hizo huku wakieleza kuwa wapo tayari kuzipokea endapo Mkurugenzi huyo hatakuwepo katika baraza hilo.


“Sisi tupo tayari kuendelea na baraza hili endapo Mkurugenzi huyu atupishe humu ndani akaendelee na kazi zake, mangapi tumezungumza kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya wananchi utekelezaji wake umekuwa ni tatizo tunataka ndani ya baraza hili atupishe aondoke”, alisema Benedict Ngwenya Diwani wa kata ya Mpepai.

Akichangia hoja katika baraza hilo naye Tasilo Ndunguru ambaye ni Diwani wa kata ya Kikolo alisema kuwa hawataki kuiona sura ya Mkurugenzi huyo katika baraza la Madiwani wa mji wa Mbinga, huku akieleza kuwa ameshindwa hata kusimamia mradi wa uvunaji msitu wa Mbambi na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kuwa naye katika halmashauri ya mji huo.

Mkurugenzi huyo pamoja na kujikuta akiwa katika wakati mgumu kwa upande wake alipopewa nafasi ya kujieleza alisema kuwa yeye akiwa Katibu wa kikao hicho, anachotambua ni kwamba kilichopo mbele ya baraza ni kupokea agenda na kwamba kama wajumbe hao wamekataa kuzipokea maana yake hakuna kikao.

“Tukiendelea kujadili yaliyopo hapa sura yangu hayatasaidia kwamba sisi ni binadamu ni kweli tumeumbwa na chuki lakini vilevile na kusamehe, mimi katika nafasi yangu ni Katibu wa kikao hiki nina hiari ya kumkaimisha mtu au kutokaimisha”, alisema Mageni.


Hata hivyo katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye pamoja na kuwasihi Madiwani hao wasifanye hivyo, lakini hawakuweza kukubaliana naye badala yake waliendelea kujenga msimamo wao wa kukataa kufanya kikao hicho na hatimaye Mwenyekiti wa baraza hilo, Ndunguru alilazimika kuvunja baraza na Madiwani walitoka nje ya ukumbi na kurudi makwao.

No comments: