Sunday, October 22, 2017

MKURUGENZI HALMASHAURI MJI WA MBINGA NA WENZAKE WATUHUMIWA KUTAFUNA MAMILIONI YA FEDHA ZA MSITU

Baraza maalum la Madiwani Halmashauri ya mji wa Mbinga likiwa limeketi katika kikao chake kujadili ubadhirifu wa fedha za mavuno ya msitu wa Mbambi katika halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati maalum ya kuchunguza msitu wa Mbambi halmashauri mji wa Mbinga, Kelvin Mapunda akikabidhi taarifa ya uchunguzi kwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ndunguru Kipwele.
Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, limetoa mapendekezo yake ya kumkataa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Robert Kadaso Mageni kwamba hawataki kufanya naye kazi tena, wakimtuhumu ametafuna fedha za mauzo ya mbao zilizopasuliwa katika msitu wa Mbambi uliopo mjini hapa ambao ni mali ya halmashauri ya mji huo.

Robert Kadaso Mageni.
Aidha imeelezwa kuwa Mkurugenzi huyo amelipotosha baraza hilo katika kikao walichoketi Novemba 2 hadi 3 mwaka jana na kutoa taarifa za uongo kwamba msitu huo una jumla ya miti 5,4040 ambayo inafaa kupasuliwa mbao wakati ukweli ni kwamba msitu ulikuwa na miti 8,470.

Kufuatia taarifa hizo ambazo hazikuwa sahihi wakati anazitoa kwenye baraza hilo juu ya uvunaji wa msitu huo, hali hiyo imesababisha halmashauri kupata hasara ya shilingi milioni 888,000,000.

Baada ya baraza hilo la Madiwani kutoa mapendekezo hayo ya kumkataa, walimtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kufikisha kilio chao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli ili aweze kuchukua hatua zaidi za kinidhamu dhidi ya mtumishi huyo.


Maamuzi hayo ya baraza hilo yalifikiwa juzi baada ya Kamati maalum iliyoundwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Nshenye kutoa taarifa yake ya uchunguzi katika baraza la dharula lililoketi juzi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, ambapo baada ya kufanya uchunguzi wake waliweza kubaini mapungufu yaliyojitokeza katika shughuli hiyo ya uvunaji wa msitu.

Akiwasilisha taarifa ya uchunguzi wa tuhuma hizo mbele ya baraza hilo ambalo lilihudhuriwa na Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga wakiwemo na Wajumbe wa kamati yake ya ulinzi na usalama, Katibu wa kamati ya kuchunguza tuhuma hizo Benedict Ngwenya ambaye ni diwani wa kata ya Mpepai alisema kuwa wamefanya kazi hiyo ya uchunguzi kwa siku 21 na kwamba walianza kubaini Mkurugenzi Mageni ameshirikiana na watendaji wake wa halmashauri ya mji huo kuhujumu mapato hayo.

Ngwenya alifafanua kuwa ufisadi huo uliofanyika, Mkurugenzi ameshirikiana na baadhi ya watendaji wake wa halmashauri ambao waliteuliwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kusimamia uvunaji wa msitu wa Mbambi ambao watendaji hao aliwataja kuwa ni Afisa misitu wa halmashauri ya mji huo, David Hyera na mlinzi mkuu Efreim Kawonga.

“Kwa msingi huo kamati ilibaini mbao nyingi ziliibwa kwa kisingizio kwamba zimekwenda kwenye shughuli ya mbio za Mwenge wa Uhuru wakati sio kweli na hata fedha zilizotokana na uvunaji huo tumefuatilia kwenye akaunti husika hakuna fedha iliyoingizwa”, alisema Ngwenya.

Alisema kuwa thamani hiyo halisi na ubadhirifu uliofanyika katika msitu wa Mbambi waliweza kuipata baada ya kamati hiyo kufanya uchunguzi wa kina kwa kuwatumia wataalamu waliobobea katika masuala ya uvunaji wa misitu ambao walitoka nje ya halmashauri ya mji wa Mbinga.

“Mapendekezo ya awali aliyoyaleta Mkurugenzi huyu Novemba 12 mwaka 2016 katika baraza lililopita la Madiwani alituambia kwamba msitu huu baada ya mavuno zingepatikana shilingi milioni 325,000,000 lakini hadi leo hii tunaambiwa mapato yaliyopatikana ni shilingi milioni 130,000,000 tu jamani kweli hata katika mtazamo wa kawaida jambo hili linaweza kuingia akilini ?”, alihoji Ngwenya.

Alieleza kuwa hasara hiyo iliyopata halmashauri kutokana na uzembe uliofanyika na watendaji hao ambao wamepewa dhamana na Serikali kusimamia shughuli za maendeleo na mali za umma, wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Ngwenya aliongeza kuwa hasara hiyo imesababishwa pia kutokana na taratibu husika zilizowekwa wakati wa kupasua mbao katika msitu huo, hazikufuatwa kwa mujibu wa sheria za nchi ikiwemo kwamba hata Mkurugenzi huyo amekiuka baadhi ya sheria ambazo zinakataza suala la Serikali kufanya biashara ya kuuza mbao badala yake ilitakiwa kuuza miti iliyopo kwenye msitu huo baada ya upembuzi yakinifu kufanyika.

Alifafanua kuwa Mkurugenzi, Mageni alipaswa kulieleza bayana baraza hilo la Madiwani kwamba Serikali haifanyi biashara ya mbao kwa mujibu wa sheria hiyo lakini alilipotosha na hakuweza kutoa ufafanua wowote ikidaiwa kwamba alikuwa na lengo la kutaka kujinufaisha yeye binafsi kupitia mauzo ya mbao hizo.

“Kama tungefuata taratibu za Serikali hasara hii tungeweza kukabiliana nayo lakini mtaalamu wa misitu, Hyera alishindwa hata kumshauri Mkurugenzi wake juu ya taratibu za zabuni za uvunaji wa msitu huu, badala yake wametumia mbinu za ujanja kumtafuta mzabuni ambaye wanamjua wao ambapo kamati hii maalum ilipofanya uchunguzi wa kina tulibaini zabuni ya kuvuna msitu ule na mikataba yake haikufuata taratibu husika”, alisema.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Ndunguru Kipwele akizungumza katika kikao hicho alisema kuwa anaipongeza kamati kwa kazi nzuri iliyofanya ya kuchunguza jambo hilo na kueleza kuwa baraza linaafiki juu ya mapendekezo yaliyotolewa kwa kuiomba Serikali ichukue hatua kali za kinidhamu dhidi ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kwa kuwa mamlaka iliyomteua ni ya Rais wa nchi.

Kadhalika alisema baraza limependekeza pia mtaalamu wake wa misitu, Hyera na mlinzi mkuu, Kawonga wafukuzwe kazi na kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria.

Alipohojiwa na waandishi wa habari, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Mageni alisema kuwa yeye hawezi kuzungumzia jambo lolote hivi sasa juu ya tuhuma hizo kama niza kweli au la.

Vilevile kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye aliipongeza kamati hiyo ya uchunguzi wa msitu wa Mbambi huku akieleza kuwa, “taarifa hii waliyoitoa hapa ni ya kweli kabisa kwa hiyo mimi niwapongeze sana na sisi kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya baada ya kutoka hapa tunayo ya kufanya”, alisema.

Hata hivyo kamati maalum iliyoshiriki kufanya kazi ya kuchunguza tuhuma hizo katika halmashauri ya mji huo ni diwani wa kata ya Bethlehemu, Kelvin Mapunda ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kamati, Benedict Ngwenya diwani wa kata ya Mpepai ambaye alikuwa Katibu na Wajumbe wengine ambao ni Simon Ponera diwani wa kata ya Kilimani, Leonard Mshunju diwani wa kutoka kata ya Matarawe, Frank Mgeni diwani wa kata ya Mbinga mjini B na Grace Millinga diwani wa viti maalum kata ya Mbinga mjini. 

No comments: