Friday, October 13, 2017

TFDA SONGEA YAKAMATA MAFUTA FEKI YA ALBINO NA VYAKULA VILIVYOHARIBIKA

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea, Mameritha Basike akionesha kwa waandishi wa habari mafuta feki ya Albino ambayo yalikamatwa katika moja ya duka linalouza vipodozi mjini hapa.
Baadhi ya vyakula vilivyoharibika na mafuta feki ya albino ambavyo vilikamatwa hivi karibuni na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Songea.
Na Albano Midelo,    
Songea.

IDARA ya Afya katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na watalaamu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wamefanya Operesheni katika maduka ya vipodozi katika mji wa Songea mkoani humo na kufanikiwa kukamata mafuta ya Albino yakiuzwa kinyume cha sheria na taratibu husika.

Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dokta Mameritha Basike alisema mafuta hayo yalikamatwa juzi katika duka la Godluck Mranga ambayo yalikuwa yanauzwa shilingi 4,500.

“Hairuhusiwi mafuta ya kupaka Albino aina ya Sunblock Cream UV40 kuwepo kwenye maduka ya vipodozi badala yake mafuta haya yanaruhusiwa kuwepo kwenye maduka ya dawa (Pharmacy)”, alisema Dokta Basike.


Alisema katika duka hilo pia vimekamatwa vyakula mbalimbali vilivyoharibika yakiwemo maziwa ya kopo 12 yenye thamani ya zaidi ya shilingi 200,000 na nyama ya kopo 20 zenye thamani ya shilingi 100,000.

Ofisa Afya wa Manispaa ya Songea Vitalis Mkomela alisema mfanyabiashara huyo ametozwa faini ya shilingi 500,000 kulingana na sheria za TFDA na kwamba ametoa rai kwa wafanyabiashara wengine kuacha kuwauzia wananchi bidhaa ambazo zimeharibika au kumalizika muda wake.

“Natoa wito kwa wananchi kabla ya kununua bidhaa yoyote wajiridhishe kwa kusoma tarehe ya kutengenezwa bidhaa na mwisho wa matumizi, ili kuepuka kununua bidhaa ambazo zimeharibika na kupita muda wake wa matumizi ambazo zinaweza kuleta athari kiafya kwa mtumiaji”, alisisitiza Mkomela.

Naye mfamasia wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Ndavitu Sanga alitahadharisha watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) katika Manispaa hiyo kuwepo kwa mafuta feki ya kupaka aina ya Sunblock Cream UV40 kwa ajili ya Albino yanayosaidia kujilinda dhidi ya Saratani ya ngozi.


Kulingana na Sanga alisema kuwa mafuta hayo feki ya Albino yamekuwa yakiuzwa kati ya shilingi 3,500 hadi 6,000 na kwamba mafuta halisi yamekuwa yakiuzwa kati ya shilingi 40,000 hadi 90,000.

No comments: