Saturday, January 27, 2018

WANAFUNZI NANDEMBO TUNDURU KUONDOKANA NA KERO UPUNGUFU WA MABWENI YA KULALA

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Homera, upande wa kulia akizungumza na baadhi ya Wanafunzi wa kike kidato cha sita shule ya Sekondari Nandembo Wilayani humo  alipokuwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule hiyo.


Na Muhidin Amri,            
Tunduru.

WANAFUNZI wanaosoma kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari Nandembo kata ya Nandembo Halmashauri Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, hivi sasa wataweza kuondokana na kero ya mahali pa kulala baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mabweni mawili yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 160 kwa wakati mmoja.

Mary Ndunguru ambaye ni Mkuu wa shule hiyo alisema kuwa ujenzi wa mabweni hayo hadi kukamilika kwake zimetumika shilingi milioni 150 kwa kutumia mfumo wa Force Account ambapo mafundi wadogo ndiyo wanaotumika kufanya kazi hiyo badala ya kutumia Wakandarasi wakubwa.

Alisema kuwa ili kuweza kutosheleza mahitaji husika kila bweni litatumiwa na watoto 50 lakini baada ya bweni moja kuungua moto mwaka jana hivi sasa wanabweni moja tu na wanafunzi wengine hulazimika kuishi kwenye hosteli za Kanisa Katoliki Nandembo kwa gharama za wazazi wao.


Ndunguru alifafanua kuwa bado shule ina uhitaji mkubwa wa mabweni kwani hata yale yanayotarajia kukamilika ujenzi wake yamejengwa kwa ajili ya matumizi ya kidato cha tano na sita, hivyo kuiomba Serikali iangalie uwezekano wa kujenga mabweni mengi zaidi yatakayoweza kulaza wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi nne nao waweze kuishi katika mazingira ya shule.

“Tunaiomba Serikali yetu iangalie uwezekano wa kutujengea mabweni haya, maabara na ukumbi wa chakula shule hii ni ya bweni lakini bado tunakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa miundombinu yake”, alisema Ndunguru.

No comments: