Monday, January 22, 2018

MADABA WAZINDUA MPANGO MAALUM KILIMO CHA ZAO LA KOROSHO

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Palolet Mgema akizungumza na baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Mbangamawe kata ya Gumbiro Halmashauri ya Wilaya ya Madaba wakati wa uzinduzi wa mpango wa upandaji zao la korosho katika halmashauri ya Madaba.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda wa pili kushoto akimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Songea, Palolet Mgema miche bora ya korosho iliyooteshwa katika vitalu kijiji cha Magingo Madaba siku ya mpango wa uzinduzi upandaji wa zao la korosho ambapo jumla ya miche 55,000 imesambazwa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali Wilayani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda upande wa kushoto akisaidiwa kupanda mche wa korosho na Mratibu wa zao la korosho, Paschal Umbu wakati wa uzinduzi wa mpango wa upandaji zao hilo uliofanyika katika kijiji cha Mbangamawe Madaba.


Na Kassian Nyandindi,       
Madaba.

MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, Palolet Mgema ameongoza Wakulima wa kijiji cha Mbangamawe kata ya Gumbiro katika Halmashauri ya Wilaya Madaba Mkoani humo, kuzindua mpango maalum wa kilimo cha zao la korosho kwa kugawa na kupanda miche zaidi ya 55,020 ya zao hilo.

Akizindua mpango huo Mgema aliwataka Wakulima wa Madaba kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika mkakati wa kufufua zao la korosho na mazao mengine makuu ya biashara kama vile pamba, chai, tumbaku na kahawa.

Alifafanua kuwa Serikali imeamua kuimarisha zao la korosho hapa nchini baada ya kuonekana limekuwa ni zao ambalo lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa na kuharakisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja.


Mgema amewaagiza maafisa kilimo wahakikishe kwamba wanatumia muda mwingi kuwasaidia wakulima mashambani na sio kukaa Ofisini kwani wakifanya hivyo itakuwa ni chanzo cha kukwamisha malengo ya Serikali katika kuinua na kuendelea kuboresha hali ya uzalishaji wa zao hilo.

“Tunampongeza Rais Dokta John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kutoa mbegu za korosho bila malipo kwa wakulima na sasa tunapaswa kutumia fursa hii kupanda miche kwa wingi ili baadaye tuweze kuzalisha korosho kwa wingi”, alisema.

Vilevile aliongeza kuwa awali zao la korosho lilikosa hamasa ya kuendelea kuzalisha kutokana na wananchi wengi kushindwa kumudu gharama ya pembejeo.

Ameagiza pia maafisa kilimo wahakikishe kwamba katika msimu huu wa kilimo kila kaya ni lazima wanakuwa na ekari mbili za shamba la korosho na kwamba aliongeza kuwa kuanzia msimu wa mwaka huu Serikali inataka kuona mazao yote ya wakulima yanauzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ili wakulima waweze kunufaika kwa kupata soko na bei nzuri ya uhakika.

Mratibu wa zao la korosho Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Paschal Umbu naye alieleza kuwa katika msimu wa mwaka huu wa 2018/2019 wanatarajia kuzalisha tani elfu 57 za korosho kutoka tani 7.441 kwa msimu uliopita kufuatia mwamko mkubwa wa wananchi kujitokeza katika kulima zao hilo.

No comments: