Monday, January 8, 2018

OFISI YA WAZIRI MKUU KUCHUNGUZA UJENZI MRADI WA MAJI MKAKO MBINGA

Na Mwandishi wetu,       
Mbinga.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Ofisi yake itatuma tume ya kuja kuchunguza malalamiko ya ujenzi wa mradi wa maji wa wananchi uliopo katika kitongoji cha Mnazi mmoja, kijiji cha Mkako kata ya Mkako Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Aidha alisema kuwa mradi huo ulianza kujengwa Machi 28 mwaka 2014 chini ya ufadhili wa benki ya dunia, kwa gharama ya shilingi milioni 718,896,533 lakini ujenzi wake umekuwa ni wa chini ya kiwango na sehemu kubwa ya fedha za mradi huo zimekwisha tumika.

Waziri Mkuu, Majaliwa alibainisha kuwa aliyekuwa Mhandisi wa idara ya maji wa halmashauri ya Wilaya hiyo, Vivian Mndolwa alichukuliwa hatua akituhumiwa kushiriki na wenzake kuhujumu mradi huo, lakini ameshangazwa hakuna kitu kinachoendelea na badala yake amehamishwa kwenda mkoa mwingine.


"Nitaleta tume kufanya kazi ya uchunguzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, haya yote mnayoyafanya ni yale ambayo hayakubaliki katika jamii na Serikali hii ya awamu ya tano hatuwezi kuyafumbia macho", alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Pamoja na mambo mengine, mradi huo wa maji Mkako ulishindwa kufunguliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Amour Hamad Amour, Mei 8 mwaka jana kwa sababu ulikuwa hauendani na viwango halisi vinavyotakiwa katika ujenzi wake.

Mradi huo ulianza kujengwa Machi 28 mwaka 2014 chini ya ufadhili wa benki ya dunia ambapo ilibidi ujenzi wake ukamilike kwa wakati mapema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu uanze kujengwa.

Kampuni iliyohusika na kazi ya ujenzi huo imetajwa kuwa ni ya Patty Interplan ya kutoka Jijini Dar es Salaam na kwamba matumizi ya fedha hizo katika mradi huo wa maji zinadaiwa kutumika vibaya ndiyo maana mradi umejengwa chini ya kiwango na wananchi wanaendelea kukosa huduma ya maji safi na salama.

No comments: