Friday, January 19, 2018

PROFESA NDALICHAKO AWASHUSHIA RUNGU MUHAS MKUU WA KITENGO ASIMAMISHWA KAZI


Na Mwandishi wetu,

UWEPO wa madai ya harufu ya ufisadi ambao unadaiwa kufanyika katika kitengo cha Manunuzi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) kumefanya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kuagiza ufanyike uchunguzi ili kuweza kuwabaini wahusika na hatimaye wachukuliwe hatua za kisheria.

Profesa Joyce Ndalichako.
Wakati hilo likiendelea kutekelezwa pia Waziri huyo ameagiza kusimamishwa kazi kwa Mkuu anayehusika na kitengo hicho, pamoja na kuchunguzwa kwa wale wote wengine watakaohusika katika sakata hilo.

Hatua hiyo iliyochukuliwa na Profesa Ndalichako ilitokea juzi alipofanya ziara yake ya kushtukiza katika taasisi hiyo, kwa lengo la kujionea na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika hapo.

Kadhalika uwepo wa ziara hiyo ulitokana na kubaini pia matumizi mabaya ya fedha za umma, ndipo ilimlazimu Waziri kufanya hivyo ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua na kukomesha hali hiyo isiweze kujirudia tena.


Profesa Ndalichako alifafanua kuwa awali aliunda Kamati ndogo iliyokuwa inafuatilia tuhuma hizo na baadaye majibu aliyoyapata yalionesha kuna harufu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika kitengo hicho cha manunuzi.

“Tunapofika kwenye suala la manunuzi kwenye taasisi hii hakuna ushindani, badala yake kazi anapewa mtu mmoja kupitia kampuni tatu tofauti, nimefanya uchunguzi wangu nimebaini kuna kampuni tatu ambazo zote zinamilikiwa na mtu mmoja ndizo zinazopata zabuni ya ununuzi katika chuo hiki, hakuna mchakato wa kushindanisha kampuni kama zinavyoagiza sheria za manunuzi Serikalini”, alisema.

Vilevile pamoja na kuagiza Wakuu wa idara kuwa makini katika uagizaji wa vitu kulingana na mahitaji, Profesa Ndalichako alisema mbele ya uongozi wa MUHAS huku akimwagiza Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho, Mariam Mwaffisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuweza kuwanasa wale wote waliohusika na vitendo hivyo.

“Ninaagiza kusimamishwa kazi kwa Mkuu huyu wa kitengo lakini si ajabu wapo wengine mapapa, Mwenyekiti nitakukabidhi makabrasha yote niliyoyapata kutokana na uchunguzi wangu, fuatilieni hata kama ni Makamu Mkuu wa chuo, kama amehusika awajibishwe msimuogope mtu”, alisisitiza.

No comments: