Friday, January 12, 2018

MKOA WA RUVUMA WAFANIKIWA KUWA NA CHAKULA CHA ZIADA AINA YA WANGA TANI 893,887

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme.
Na Kassian Nyandindi,        
Songea.

MKOA wa Ruvuma  umefanikiwa kuvuna chakula aina ya wanga tani 1,232,776 katika msimu wa kilimo wa 2016/2017 wakati  mahitaji halisi ya wakazi wa mkoa huo ni tani 338,889 hivyo kuwa na ziada ya chakula tani 893,887.

Mkuu wa mkoa huo, Christine Mndeme alisema hayo hivi karibuni wakati wa kikao cha  Kamati ya ushauri cha mkoa (RCC) kilichofanyika mjini Songea.

Aidha  alisema kuwa ununuzi wa mahindi katika msimu wa 2016/2017 mkoa wa Ruvuma umepangiwa kununua tani 11,483 za mahindi toka kwa wakulima kwa bei ya shilingi 500 kwa kilo kupitia kwa Wakala wa  Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA).


Alisema changamoto iliyopo sasa ni uchache wa kiwango cha tani hizo ilizopangiwa mkoa huo kulingana na hali halisi ya uzalishaji, jambo lililosababisha wakulima wengi kubaki na kiasi kikubwa cha mahindi majumbani mwao.

Mndeme aliwasihi wakulima kuendelea kutafuta masoko ya uhakika ya mahindi ili kuepukana na walanguzi wakati jitihada za kuomba nyongeza ya mgawo wa Serikali zikiendelea.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa uzalishaji  huo wa chakula umetokana na matumizi bora ya pembejeo za kilimo na kuongeza kuwa, Serikali katika msimu 2017/2018 itatumia mfumo wa bei elekezi kununua pembejeo hususan mbolea ya kupandia (DP) na UREA kwa ajili ya kukuzia.

Alifanua kuwa Wizara ya kilimo pamoja na mamlaka ya udhibiti wa ubora wa mbolea Tanzania imekwishatoa bei elekezi kwa kila wilaya na mkulima atanunua mbolea kwenye duka la wakala kwa bei iliyopangwa.

Alitoa wito kwa Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo, kuhakikisha kwamba wanasimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa bei elekezi ili wakulima hao wapate mbolea kwa mujibu wa bei ya Serikali.

Lengo la Serikali ni kuona kila mkulima anatumia mbegu na mbolea ili kuongeza tija katika uzalishaji na Serikali itahakikisha inachukua hatua kali za kisheria kwa wakala au mfanyabiashara atakayeuza pembejeo za kilimo zaidi ya bei iliyoelekezwa.

Mndeme aliongeza kuwa mwezi huu mvua zimekwisha anza kunyesha katika maeneo mbalimbali na kuwaagiza maafisa ugani na wataalamu wote wa kilimo kuwatembelea wakulima mara kwa mara mashambani na kuwaelimisha juu ya mbinu za kilimo bora.

No comments: