Thursday, January 18, 2018

NAIBU WAZIRI WA UJENZI AMTAKA MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI DARAJA MTO RUHUHU NYASA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu kukifanyia ukarabati kivuko cha MV Ruhuhu kinachotoa huduma kati ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma na Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe ili kiweze kuendelea kutoa huduma kipindi chote wakati ujenzi wa daraja hilo unaendelea kufanyika.

Muonekano wa daraja la mto Ruhuhu linalojengwa Wilayani Nyasa na Mkandarasi wa Kampuni ya Lukolo kwa gharama ya shilingi bilioni 6, daraja hilo litaunganisha Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma na Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe.


Na Kassian Nyandindi,       
Nyasa.

NAIBU Waziri wa ujenzi, Elias Kwandikwa amemtaka mkandarasi anayejenga daraja la mto Ruhuhu Wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kwamba anamaliza ujenzi wa daraja hilo kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Kwandikwa alitoa agizo hilo alipokuwa Wilayani humo akikagua ujenzi wa daraja hilo ambapo ameusisitiza Uongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Makao makuu, kuhakikisha kwamba utaratibu wa zoezi zima la ununuzi wa vyuma vitakavyowekwa juu ya daraja hilo unaenda sambamba na makadirio ya muda wa mradi ili kufanya kazi hiyo ikamilike kwa muda uliopangwa.

“Nafikiri sasa jipangeni vizuri ili masika yanapokwisha mhakikishe mnafanya kazi kwa bidii ya hali ya juu, nataka kufikia mwezi Juni mwaka huu daraja liwe limekamilika, pia TANROADS Makao makuu hakikisheni mchakato wa manunuzi ya vyuma vya daraja hili mnauanza mapema ili kuweza kukamilisha mapema”, alisisitiza.


Vilevile alieleza kuwa daraja hilo ujenzi wake utakapokuwa umekamilika utakuwa ni kiungo muhimu kwa watu wa Nyasa Mkoani Ruvuma na Ludewa Mkoa wa Njombe, kwani wamekuwa wakilisubiri daraja hilo kwa ajili ya kujiendeleza katika shughuli zao mbalimbali za kukuza uchumi.

Pia amemwagiza Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoani Ruvuma, Mhandisi Elisha Mgira, kuhakikisha kwamba anarekebisha kasoro zilizopo kwenye kivuko cha mto Ruhuhu ili kuweza kufanya kazi hasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wanasubiri ujenzi wa daraja hili ukamilike.

Kwa upande wake Mhandisi Mkazi wa daraja hilo, Mhandisi Napegwa Kiseko naye alisema kuwa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 50 ambapo kazi zinazofanyika hivi sasa ni kujaza matabaka ya barabara zinazoingia darajani hapo ili kunyanyua tuta la barabara.

Napegwa alifafanua kuwa kazi hiyo inaendelea pande zote mbili yaani mkoa wa Ruvuma na Njombe, ingawa kwa kipindi hiki cha mvua kazi hiyo imekuwa na vikwazo vingi.

Alisema kuwa ujenzi wa misingi ya daraja kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma upo kwenye hatua za mwisho na Njombe ujenzi ulianza mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana na bado unaendelea.

Mradi wa ujenzi wa daraja la mto Ruhuhu ambao upo mpakani mwa Mkoa wa Ruvuma na Njombe unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 6 ambazo ni fedha za Serikali kwa asilimia mia moja na unatarajiwa kukamilka mwezi Juni mwaka huu.

No comments: