Wednesday, January 17, 2018

TBA YAENDELEA NA UJENZI WA OFISI YA DC NA DED NYASA


Na Muhidin Amri,     
Nyasa.

WAKALA wa majengo Tanzania (TBA) kupitia kikosi chake cha ujenzi Mkoani Ruvuma, ameanza kazi ya ujenzi wa miradi minne ya majengo ya Serikali Wilayani Nyasa Mkoani humo ambayo miradi hiyo inagharimiwa na Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Meneja wa TBA Mkoani hapa, Mhandisi Edwin Mnunduma alifafanua kuwa miradi yote minne inatekelezwa kwa kutumia rasilimali zilizopo Serikalini kupitia wataalamu waliopo katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya na Wakala wa majengo TBA.

Aidha alisema kuwa kikosi cha ujenzi huo kinajenga majengo yake kwa kutumia njia ya kubuni na kujenga kwa pamoja ili kuweza kutekeleza miradi ya Serikali kwa gharama nafuu.


Mnunduma alitaja miradi hiyo minne ni Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, nyumba ya makazi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri na Kituo cha afya kilichopo katika kata ya Kihagara.

Alibainisha kuwa mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambao ni wa ghorofa moja ulianza tangu mwezi Mei mwaka jana na matarajio yake ni kukamilisha kazi hiyo mwezi Februari mwaka huu.

Kutokana na upatikanaji wa fedha kwa awamu, mradi huo hivi sasa upo katika awamu ya kwanza ambapo gharama zilizotumika ni shilingi milioni 199.9 na malipo husika yamekwisha fanyika.

Mhandisi huyo alibainisha kuwa mpaka sasa malipo yaliyokwisha fanyika kwa Wakala ni shilingi milioni 80.7 sawa na asilimia 50 ya mkataba na kazi zilizofanyika ikiwemo ujenzi wa nguzo, miamba mlalo, kuezeka paa na uwekaji wa mabomba ya nyaya za umeme kwenye sakafu.

Alisema gharama za ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa hadi kukamilika kwake yamefanyika makadirio kufikia kiasi cha shilingi milioni 896.8 huku ujenzi wa ghorofa nyumba ya makazi nao utagharimu shilingi 341.3, Ofisi ya Mkurugenzi shilingi bilioni 3.28 na Kituo cha afya Kihagara ujenzi wake utakuwa ni wa shilingi milioni 585.5.

No comments: