Sunday, January 7, 2018

WIZI WA MAMILIONI YA FEDHA ZA MSITU WA MBAMBI MBINGA KUCHUNGUZWA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

SAKATA la wizi na matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha za mradi wa uvunaji wa msitu wa Mbambi katika Halmashauri ya mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, limechukua sura mpya baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kueleza kuwa ataunda tume ambayo itakuja kuchunguza jambo hilo na wahusika watakaopatikana waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Majaliwa alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Mbinga mjini, huku akieleza kuwa tume hiyo wakati wowote kuanzia sasa itawasili katika halmashauri hiyo kwa ajili ya kuanza kufanya kazi hiyo.

"Tulipokea malalamiko yenu ya idadi ya miti na tathimini mliyoifanya katika msitu ule, lakini hata mapato ya fedha zilizotokana na msitu huo hayaeleweki yaliko,


"Waheshimiwa Madiwani fanyeni kazi yenu nitaleta uchunguzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, kama kuna mtumishi yeyote atahusika au awe Mkurugenzi mtendaji tupo tayari kumchukulia hatua na huu ndiyo msimamo wetu wa Serikali ya awamu ya tano",  alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema kuwa Serikali haitaki kuona au kusikia mtumishi wa umma anakuwa mrasimu katika kuwatumikia wananchi na kwamba haitasita kuchukua hatua kwa mtumishi ambaye ataonekana anakwenda kinyume na matakwa yaliyowekwa.

Pia aliongeza kuwa katika halmashauri hiyo ya mji wa Mbinga anayotaarifa kwamba kumekuwa na migongano mingi kati ya Madiwani na watumishi ambayo imekuwa ikichangia kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Kufuatia hali hiyo amewataka kumaliza migogoro hiyo na kujenga ushirikiano ambao utaweza kuleta tija katika jamii kwa kuwa wabunifu wa kuwaletea maendeleo wananchi.

Awali hivi karibuni kufuatia sakata hilo la uvunaji wa msitu huo, baraza la Madiwani la halmashauri hiyo lilitoa pendekezo lake la kumkataa Mkurugenzi huyo wa halmashauri hiyo, Robert Kadaso Mageni kwamba hawataki kufanya naye kazi tena wakimtuhumu ametafuna fedha za mauzo ya mbao zilizopasuliwa katika msitu huo na kulipotosha baraza kwa kutoa taarifa za uongo juu ya mapato yaliyotokana na uvunaji uliofanyika huko msituni.

Kufuatia upotoshaji huo, Mageni anatuhumiwa kulidanganya baraza hilo na kusababisha halmashauri iweze kupata hasara ya shilingi milioni 888,000,000 huku Madiwani hao wakiiomba Serikali imchukulie hatua kali za kisheria.

Maamuzi hayo ya baraza hilo yalifikiwa baada ya Kamati maalum iliyoundwa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kutoa taarifa yake ya uchunguzi katika baraza la dharula lililoketi Novemba 20 mwaka jana kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, ambapo baada ya kufanya uchunguzi wake waliweza kubaini mapungufu yaliyojitokeza katika shughuli hiyo ya uvunaji wa msitu.

No comments: