Thursday, January 18, 2018

RC IRINGA ATEKELEZA AGIZO LA RAIS MAGUFULI

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza.


Na Mwandishi wetu,   
Iringa.

SIKU moja baada ya Rais Dokta John Pombe Magufuli, kupigilia msumari wa mwisho juu ya suala la michango kwa wanafunzi mashuleni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amewataka walimu wakuu wa shule zote Mkoani humo kuandika barua kueleza aina ya michango iliyopo shuleni kwao na sababu za uwepo wake.

Masenza ameonya mwalimu ambaye atatoa taarifa za uongo katika barua yake hatua kali zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo ya kuondolewa katika nafasi yake ya kazi.

“Kwenye waraka ambao kila mtu anao unazungumzia elimu bila malipo, tayari Serikali ilishaelekeza namna ya kuendesha elimu bila malipo, waraka namba 3 wa mwaka 2016 ambao unazungumzia elimu bila malipo na waraka wa elimu namba 8 wa mwaka 2011 kuhusu michango mbalimbali wanayopaswa kutoa wazazi kupitia kamati na bodi za shule,


“Mimi ninajua katika kamati na bodi za shule ninyi ni makatibu, ikifika katika jambo hili tafadhali kila mwalimu aone hahusiki na jambo lolote linalozungumzia michango katika shule za msingi na sekondari na kama kuna hitaji lolote libainishwe na jamii”, alisema Masenza.

Alifafanua kuwa shule ni za jamii na jamii ikibainisha yenyewe nje ya utaratibu wa mwalimu mkuu juu ya nini wanataka kufanya na kusimamia wao wenyewe hilo linaruhusiwa.

“Sasa nimewaita ili nijiridhishe, nitamtaka kila mwalimu mkuu wa shule kwa mkono wake mwenyewe aandike barua ya kueleza kama shule yake ina mchango ama la na barua zote ziandikwe kwa mkuu wa mkoa”, alisema.

Masenza alieleza kuwa barua hizo zitapitiwa na Ofisi yake na kisha ukaguzi utafanyika katika kila shule zikihojiwa kamati na bodi za shule kubaini michango kama ipo sababu za uwepo na namna amehusika kuwepo kwa michango hiyo.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa wa Iringa amewaagiza wakuu wa shule kuwapokea wanafunzi wote wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza bila kujali wana sare za shule au la.

Katika hatua nyingine amewataka wakuu wa shule zote za binafsi mkoani humo kuwarejesha wanafunzi waliowaondoa shuleni mwao kutokana na kutofikia wastani wa ufaulu wanaoutaka la sivyo shule zao zitafungwa.

No comments: