Friday, January 19, 2018

DOKTA MAGUFULI ASIMAMISHA USAJILI WA MELI HAPA NCHINI

Dokta John Pombe Magufuli.


Na Mwandishi wetu,

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli ametoa agizo la kusitishwa kwa usajili wa meli mpya hapa nchini, kufuatia taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya na bidhaa nyingine zinazopingwa kimataifa katika meli hizo ambazo zinapeperusha bendera ya Tanzania na sasa zimefikia tano.

Dokta Magufuli ametoa agizo hilo jana kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume.

Kadhalika amemtaka Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo na kuhakikisha jina la Tanzania halichafuliwi ndani na nje ya nchi.


Pia taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imeeleza kuwa agizo hilo lilitolewa wakati Rais akifanya mazungumzo na wafanyakazi wa Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) ambapo mawaziri hao nao walikuwepo.

“Kafanyeni uchunguzi wa kina kwa meli zote zinazopeperusha bendera ya Tanzania, fanyeni uchunguzi kwa meli zilizokamatwa ambazo ni tano na pia hizi 470 zilizosajiliwa na zinaendelea kufanya kazi zichunguzeni, hatuwezi kuacha jina la nchi yetu lichafuliwe na watu wanaofanya mambo kwa maslahi yao”, alisema Dokta Magufuli.

Vilevile alihimiza kutekelezwa kwa maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu, ambaye alitangaza kuzifutia usajili wa meli mbili zilizokamatwa sanjari na kuamuliwa kushusha bendera ya Tanzania.

Suluhu alizitajia meli hizo kuwa ni Kaluba yenye usajili wa namba IMO6828753 iliyokamatwa maeneo ya Jamhuri ya Dominican Desemba 27 mwaka jana, ikiwa na wastani wa tani 1.6 ya dawa za kulevya pamoja na Andromeda yenye namba za usajili IMO 7614666 iliyokamatwa ikisafirisha silaha kinyume na sheria za kimataifa.

No comments: