Wednesday, January 24, 2018

WAKULIMA TUNDURU WAISHUKURU SERIKALI UGAWAJI MICHE BURE YA KOROSHO

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Juma Homera upande wa kushoto akijifunza namna ya uandaaji wa miche bora ya korosho kwa njia ya kuotesha kutoka kwa mkulima wa zao la korosho ambaye hakutaka kutaja jina lake.


Na Muhidin Amri,                
Tunduru.

WAKULIMA wanaozalisha zao la korosho Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma wameipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Rais Dokta John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wake wa kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha na  kuimarisha zao hilo kwa kuzalisha  miche ambayo inatolewa bure kwa wananchi.

Walisema kuwa hatua hiyo itahamasisha wananachi wengi kuanza kulima zao hilo na kuweza kujikwamua na umaskini kwa kuwa Serikali imeonesha dhamira ya dhati katika kuwasaidia wakulima.

Kwa nyakati tofauti wakizungumza na mwandishi wetu walisema kuwa hiyo ni hatua nzuri kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani imeonesha ni jinsi gani inavyowajali wananchi wake hasa kwa kuondoa baadhi ya kero za muda mrefu ambazo zilikuwa zikiwakatisha tama wakulima na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo.


Lwiza Mkuha na Ali Said mbali na pongezi hizo waliiomba Serikali kuangalia na mazao mengine ikiwemo karanga na mpunga ambayo yanalimwa na kustawi vizuri katika Wilaya hiyo kwa kutoa mbegu bora ili kuongeza uzalishaji wake.

Mkuha alisema kuwa walikuwa hawafahamu kama Halmashauri ya Wilaya imeandaa mpango huo wa kutoa miche bora ya korosho na kuwataka wakulima wenzake kuchangamkia fursa hiyo ambayo inaonekana itawaondoa wakulima wa Wilaya ya Tunduru katika umaskini.

Pia amewataka wanawake wengine wa Wilaya hiyo kuacha kubweteka kwa kuwa tegemezi badala yake waanze sasa kulima zao la korosho ambalo hapo baadaye litawaondolea aibu na dharau ya wanaume kwa kuwaita majina mengi ya ajabu ambayo yanawavunjia utu wao.

No comments: