Thursday, January 11, 2018

MAJALIWA: WIZARA INAYOHUSIKA NA MASUALA YA UTALII INAOWAJIBU WA KUANZISHA MAMLAKA ZA FUKWE KWENYE BAHARI NA MAZIWA

Baadhi ya Wavuvi wakiwa katika ziwa Nyasa wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,      
Nyasa.

SERIKALI imeagiza kuwa, Wizara inayohusika na masuala ya utalii inaowajibu wa kuanzisha mamlaka za fukwe kwenye bahari na maziwa, ili kuweza kuimarisha shughuli za utalii hapa nchini.

Agizo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambapo alisema kuwa kuanzishwa kwa mamlaka hiyo kutasaidia kuboresha utalii maeneo ya fukwe na kuhamasisha watu mbalimbali waweze kufanya uwekezaji kwa kujenga hoteli kubwa kwenye fukwe hizo sambamba na kuwafundisha wananchi namna ya kuwapokea watalii kwa ukarimu ili waweze kurudi kutalii siku za mbele.

Majaliwa alisema hayo wakati wa uzinduzi wa Tamasha la utalii lililofanyika hivi karibuni ufukweni mwa ziwa Nyasa mjini Mbamba bay ambalo lilibeba ujumbe wenye kauli mbiu isemayo, Tangaza utalii na fursa za uwekezaji Nyasa kuelekea uchumi wa viwanda.


Tamasha hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali kutoka ndani ya wilaya za mkoa huo.

Alisema jukumu kubwa walilonalo wananchi wa Wilaya ya Nyasa ni kuhakikisha kwamba wanatunza mazingira ya fukwe kwa kuyafanyia usafi na kuhamasisha wawekezaji mbalimbali kwenda kuwekeza kwenye maeneo hayo na kwamba Serikali itaendelea kuandaa mazingira mazuri ambayo yatawavutia wawekezaji hao ikiwemo kujenga barabara ya lami kutoka Mbinga mjini hadi Mbamba bay mradi ambao tayari mkandarasi amepatikana.

“Endeleeni kuitangaza Nyasa, anzeni wenyewe sisi tutaunga mkono kwa nguvu zote ikiwemo kujenga barabara kutoka Mbinga mjini hadi hapa Nyasa kwa kiwango cha lami sambamba na kuendelea kupeleka umeme hadi vijijini jambo ambalo litakuwa kivutio kikubwa kwa watalii", alisisitiza Majaliwa.

Majaliwa alisema moja kati ya lengo la Serikali ni kuhakikisha kuna kuwa na meli nzuri ya kubeba abiria na meli ya mizigo ambapo napo uwepo wake utasaidia kuwavutia watalii wa ndani na nje na kwamba kinachotakiwa wananchi wanapaswa kuhakikisha wanajibidiisha pia katika shughuli za ujasiriamali kwa kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo vikundi vitakavyojihusisha na masuala ya uvuvi ili iwe rahisi kupata mikopo ambayo imekuwa ikitolewa na halmashauri ya wilaya hiyo kupitia mapato yake ya ndani.

“Nimesikia ziwa hili ndilo lenye aina nyingi ya samaki kuliko aina zote za maji baridi ikiwa ni aina tofauti za samaki, taarifa ya Wizara ya uvuvi na maendeleo ya mifugo nchini inaonesha kuwa samaki wanaovuliwa kwa ajili ya biashara ya samaki wa mapambo kutoka ziwa Nyasa wamegawanyika katika makundi mawili makubwa ambayo ni samaki wale wanaoishi zaidi kwenye mawe au miamba ambao kuna aina zipatazo 250,

“Lakini kundi la pili ni samaki ambao hawapendelei kuishi kwenye mawe na ambao pia wengi wao hutumika kwa kitoweo na wako chini ya koo 38, hata hivyo utafiti bado unaendelea kufanyika ili kubaini wingi na idadi ya samaki wa mapambo katika ziwa Nyasa kupitia taasisi yake ya utafiti TAFIRI", alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu huyo alisema kwamba utajiri huo mkubwa uliopo kwenye ziwa hilo unapaswa kutumiwa vizuri ili wavuvi waweze kunufaika hivyo Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za vikundi vya ujasiriamali nchini ikiwemo vikundi vya wavuvi.

No comments: