Thursday, January 4, 2018

DC: KUENDELEA KUSHAMIRI UCHAFU MJI WA MBINGA KUNATOKANA NA UZEMBE WA MKURUGENZI MTENDAJI


Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye akizungumza na Waandishi wa habari jana (Hawapo pichani) juu ya hali ya mji wa Mbinga kuwa mchafu ambapo alilalamikia Mkurugenzi na Watendaji wa mji huo kutowajibika ipasavyo.
Hili ni moja kati ya ghuba la uchafu lililopo katika Mji wa Mbinga katika mtaa wa Msikitini katikati ya makazi ya watu ambalo wakazi wa mji huo hulamimikia hali hiyo kwa kukaa kwa muda mrefu bila kuzolewa taka na kuleta kero katika jamii.















Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa kitendo cha Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma kuendelea kushamiri uchafu, kunatokana na uzembe unaofanywa na Mkurugenzi mtendaji wa mji huo, Robert Kadaso Mageni au Watendaji wake ambao wamepewa dhamana ya kusimamia na kutekeleza jambo hilo.


Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake akitolea ufafanuzi juu ya kutozolewa uchafu kwa wakati, kwenye maghuba ya kuhifadhia taka yaliyopo mjini hapa.


“Ninakiri suala la mji kuwa mchafu, uhamasishaji wa watu kuuweka mji katika hali ya usafi umekuwa mdogo hivyo wanapaswa kuendelea kutekeleza hili hatutaki kuona maghuba yana uchafu, kiutendaji sio sahihi kila leo unapewa maelekezo”, alisema Nshenye.


Alisisitiza kuwa zoezi hilo linapofanyika hususan kila jumamosi ya mwisho wa mwezi wanatakiwa pia washirikishe wadau mbalimbali na kwamba haitakiwi katika maghuba hayo taka hizo kukaa kwa muda mrefu.



Katika hatua nyingine, Nshenye alishangazwa na Mkurugenzi huyo kuendelea kuwa na tabia isiyokuwa nzuri ya kuwakimbia waandishi wa habari na kuwaona maadui, hasa pale wanapohitaji majibu au ufafanuzi wa jambo fulani katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya wananchi.



Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa kwa yale mambo ambayo waandishi wa habari wanayahitaji anapaswa kuyatolea ufafanuzi na sio kutumia lugha ambazo sio nzuri, ukizingatia kwamba yeye ni kiongozi ambaye amepewa dhamana na Serikali katika kuwatumikia wananchi.


“Kiutendaji sio sahihi kila leo umekuwa mtu wa kulalamikiwa na kupewa maelekezo, mimi ninachotambua waandishi wanapohitaji ufafanuzi wa jambo fulani ni lazima aseme na sio kuwakimbia”, alisisitiza Nshenye.

No comments: