Saturday, January 27, 2018

UGONJWA WA NGURUWE WASUMBUA SONGEA


Na Albano Midelo,      
Songea.

UGONJWA hatari wa homa ya nguruwe umeingia katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ambapo hadi sasa zaidi ya nguruwe 100 wamekufa.

Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Rozina Chuwa amesema kuwa katika kipindi cha wiki mbili, vimetokea vifo hivyo 100 vya nguruwe na kwamba hadi kufikia Jumapili iliyopita nguruwe 48 walikuwa wamekufa kutokana na ugonjwa huo.

Chuwa alisema kuwa ugonjwa huo unaenezwa virusi aina ya ‘African Swine Fever Virus’ na kwamba hauna kinga na unaenea kwa kasi kubwa katika Manispaa hiyo yenye jumla ya nguruwe 4,581 ambapo ametaja maeneo ambayo yanaongoza kuathirika na ugonjwa huo ni Lizaboni ambako nguruwe zaidi ya 100 wamekufa.


Maeneo mengine ambayo yameripotiwa kuingia ugonjwa huo mwezi huu Januari 24 hadi 25 mwaka huu katika kipindi cha mwaka huu ni Ruhuwiko, Mshangano na Mjimwema.

“Kwa kuwa ugonjwa huu wa homa ya nguruwe hauna kinga, kitaalamu inashauriwa njia rahisi ya kukabiliana nao ni kuchinja nguruwe ambao wapo katika maeneo ambayo umetokea ugonjwa huo ambao unaua nguruwe kwa kas”, alisema.

Kadhalika alieleza kuwa njia hiyo inakuwa ngumu kutekelezeka kwa sababu wananchi wengi hawakubali kuchinja nguruwe wao, hali ambayo inasababisha ugonjwa huo kuenea kutokana na kununua nyama ya nguruwe wenye ugonjwa.

Alisema ugonjwa huo haina madhara kwa binadamu ambapo kitaalam nguruwe aliyekufa kwa ugonjwa huo anatakiwa kuzikwa katika shimo lililopuliziwa dawa lenye urefu wa zaidi ya meta moja.

“Sisi kama wataalam wa afya ili kudhibiti ugonjwa wa homa ya nguruwe tunashauri kuzuia kabisa biashara ya nyama ya nguruwe kwa sababu ugonjwa huu hauna kinga kwa nguruwe”, anasisitiza Chuwa.

No comments: