Wednesday, January 24, 2018

DC TUNDURU AIOMBA WIZARA YA MAJI KUSAIDIA UTEKELEZAJI MIUNDOMBINU YA MAJI


Na Kassian Nyandindi,      
Tunduru.
 
SERIKALI Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma, imeiomba Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuangalia uwezekano wa kuipatia Wilaya hiyo fedha shilingi milioni 300 ambazo iliomba, kwa ajili ya kusaidia kuharakisha utekelezaji wa ujenzi miundombinu ya maji katika mji wa Tunduru.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Homera alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake juu ya maendeleo mbalimbali ya ujenzi wa miradi ya maji katika mji huo.

Homera alifafanua kuwa maombi hayo yalitokana na Mamlaka ya maji mjini hapa kuelemewa na ubovu wa miundombinu yake hali ambayo husababisha wananchi kutumia maji yasiyokuwa safi na salama.


Alisema kuwa fedha hizo ni maombi ya mwaka wa bajeti wa 2017/2018  kwa Wizara hiyo, kwa ajili ya kuweza kusaidia kuboresha miundombinu hiyo ili kuweza kufikia lengo la asilimia 90 ya upatikanaji wa maji hayo.

Vilevile Mkuu huyo wa Wilaya aliishukuru Wizara kwa kuipatia Wilaya ya Tunduru kwa kuipatia fedha shilingi milioni 300 katika bajeti yake ya mwaka 2016/2017 ambayo imewezesha kuongeza na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 40 hadi kufikia asilimia 60.

Alisema kuwa fedha hizo zilitumika kuimarisha miundombinu ya maji katika mji huo kwa kusambaza mtandao mpya wa mabomba ya maji wenye urefu wa kilometa tisa na kufanya mtandao huo kufikia kilometa 34 tofauti na awali ambapo ulikuwa na urefu wa kilometa 25.

“Tukipata fedha hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza tatizo la maji katika mji wetu wa Tunduru, bado tunayoshida katika sekta hii ya maji na Serikali sasa inaendelea kuhakikisha inamaliza changamoto zilizopo ili wananchi watumie muda wao kwa ajili ya kufanya kazi za kukuza uchumi badala ya kuhangaika muda mwingi kutafuta maji mbali na makazi yao”, alisema Homera.

Pia akizungumzia utekeleza wa miradi  ya maji katika vijiji mbalimbali  vilivyopo wilayani humo, alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo imeweza  kuchimba visima virefu 35 ikiwa ni juhudi za Mkuu huyo wa wilaya kuhakikisha kwamba anasogeza huduma bora ya maji karibu na wananchi.

Katika utekelezaji huo Halmashauri ya wilaya hiyo kupitia mapato yake ya ndani, fedha kutoka Serikali kuu katika kipindi cha miaka miwili imetumia zaidi ya shilingi milioni 112 kwa ajili ya kufanikisha uboreshaji wa miundombinu ya maji, kwenye vijiji na Kata mbalimbali Wilayani humo.

Alisema kuwa fedha hizo zilitumika kuchimba visima virefu, kukarabati na kufunga mashine za kusukuma maji katika shule za Sekondari, zahanati pamoja na vituo vya afya kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa huduma husika.

Kadhalika katika utekelezaji huo wadau wa maendeleo kupitia shirika la AMCC kutoka nchini Canada wamechimba visima 25 katika vijiji 67 vilivyopo katika kata 16 Wilayani Tunduru na kusaidia kupunguza tatizo la maji kutoka asilimia 40 hadi 75.

Hata hivyo aliongeza kuwa kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo wananchi wengi walikuwa wakichota maji katika mito na visima vifupi wakinyang’anyana na wanyama wakali kama vile simba, tembo, chui, nyoka na fisi.

No comments: