Sunday, January 7, 2018

WAKULIMA WA KAHAWA MBINGA KUSAJILIWA KWENYE MFUMO UTOAJI TAARIFA ZA MASOKO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akiwa katika eneo la Kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga wakati alipotembelea juzi kwa lengo kujionea maendeleo ya kiwanda hicho.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameitaka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kuwawezesha wakulima wanaozalisha zao la kahawa Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wajisajili kwenye mfumo wa utoaji wa taarifa za masoko ya dunia ili mauzo ya kahawa yao yaendane na soko hilo.

Agizo hilo la Waziri Mkuu, Majaliwa alilitoa juzi wakati alipokuwa ametembelea na kukagua Kampuni ya Kiwanda cha Kukoboa Kahawa Mbinga (MCCCO) iliyopo Wilayani humo.

Pia alisema kuwa ili kuwawezesha wakulima hao waweze kuuza kahawa yao moja kwa moja mnadani bila kupitia kwa mtu binafsi ni lazima waingizwe kwenye mfumo huo ili watambue soko la dunia lipoje.


Alisema kuwa kwa kufanya hivyo kutawafanya wakulima wa kahawa kuepukana na wafanyabiashara wajanja ambao huwatapeli fedha zao kupitia mauzo ya kahawa yao mnadani.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya kahawa Tanzania, Primus Kimaryo alimthibitishia Waziri Mkuu, Majaliwa kuwa bodi hiyo inao uwezo wa kusimamia hilo na wakulima wataweza kuingizwa kwenye mfumo wa kupata taarifa za soko la dunia kwa wakati.

Alisema kuwa namna ya kuweza kujisajili na mfumo huo ni gharama ya dola za Kimarekani 1,000.

Pamoja na mambo mengine awali naye Meneja wa MCCCO Wilayani Mbinga, Jonas Mbunda aliiomba Serikali kuweka sera itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kwa wakulima pamoja na uhamasishaji unywaji wa kahawa ya ndani ya nchi.

Alisema Serikali inatakiwa kuhakikisha kwamba inatafuta masoko ya uhakika kwa ajili ya kuwafanya wakulima hao waweze kuuza kahawa yao kwa bei nzuri.

Mbunda alimweleza Waziri Mkuu, Majaliwa kuwa endapo itasimamia mambo hayo maendeleo ya uzalishaji wa zao la kahawa wilayani Mbinga yatakuwa juu na hatimaye kuweza kufikia malengo husika.

Alisema kuwa MCCCO mkakati walionao hivi sasa katika kujiongezea mapato ni kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake ili kuweza kupata kiasi cha kahawa kinachozidi asilimia 60 ambazo wanazipata hivi sasa.

Vilevile mkakati mwingine walionao ni kujenga kiwanda kidogo cha kusindika kahawa ya kunywa ambayo huyeyuka mara moja pamoja na kuendelea na biashara ya ununuzi wa kahawa bora.

"Mheshimiwa Waziri Mkuu kiwanda hiki kinao uwezo wa kukoboa tani 12 za kahawa kwa saa na 30,000 katika msimu kwa mwaka, lakini tukiangalia kwenye orodha ya mapokezi wakati kiwanda kimeanza 1989 hadi sasa 2018,

"Hakuna uwezo wa kupokea kahawa zaidi ya tani 10,000 tumekuwa tukipokea tani 5,000 hadi 10,000 maana yake ni kwamba kinafanya kazi chini ya uwezo wake kutokana na uzalishaji wa kahawa hapa Mbinga kuwa kidogo", alisema Mbunda.

Meneja huyo alisema kuwa hali ya uchumi wa kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga kutoka mwaka 2012 hadi 2017 kinaendeshwa kwa faida na kwamba hakijawahi kupata hasara katika kipindi hicho cha miaka mitano.

Mbunda aliongeza kuwa kiwanda kimekuwa kikilipa kodi zote za Serikali na kimeweza kupata hati tuzo ya kuwa mlipa kodi mkubwa katika ngazi ya wilaya kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.

Hata hivyo Kampuni ya kiwanda cha kukoboa kahawa Wilayani Mbinga inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia  43 na asilimia 57 kutoka kwenye vyama vya ushirika vinavyolima zao la kahawa hapa nchini. 

No comments: