Tuesday, January 2, 2018

MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI MJI WA MBINGA ATUHUMIWA KUKWAMISHA UKAMILISHAJI UJENZI MRADI WA KITUO CHA AFYA KALEMBO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli.

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

AGIZO la Serikali la kutaka kujengwa na kukarabatiwa kwa vituo 172 vya afya kote nchini na kuhakikisha kwamba kazi hiyo iwe imekamilika ifikapo Desemba 30 mwaka huu, hali hiyo imekuwa kinyume kwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma ambapo mpaka sasa ujenzi wa Kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu ndani ya halmashauri hiyo haujakamilika.

Hilo limebainika kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Diwani wa kata hiyo, Dustan Ndunguru na wananchi wake wakieleza kuwa licha ya kituo hicho kupewa fedha zaidi ya shilingi milioni 500 lakini hali ya maendeleo ya ujenzi wake imekuwa ikifanyika kwa kusuasua.

Diwani huyo na wananchi wake wamemlalamikia Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Robert Kadaso Mageni wakimtuhumu kwamba ndiye aliyesababisha na kukwamisha kutokamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kwa wakati uliopangwa kulingana na agizo lilitolewa na Serikali.

Ndunguru alisema kuwa Serikali licha ya kuwataka viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa kuhakikisha wanasimamia kazi hiyo iwe imekamilika ifikapo Desemba 30 mwaka jana na baada ya hapo, iweze kuweka vifaa tiba vya kuweza kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya hali hiyo imekuwa kinyume hivyo aliongeza kuwa kuna kila sababu ya mamlaka husika ngazi ya juu Serikalini kuchukua hatua ili iweze kuwa fundisho kwa viongozi wengine ambao ni wazembe katika kusimamia miradi ya maendeleo ya wananchi.

Alisema kuwa tokea ujenzi huo uanze kufanyika katika kata yake ya Kihungu kumekuwa na uzembe mkubwa ukifanyika wa uagizaji wa vifaa vya ujenzi na malipo kwa mafundi waliokuwa wakifanya kazi ya ujenzi jambo ambalo lilisababisha hata baadhi yao kugoma kuendelea kufanya kazi.

“Pamoja na Serikali kutaka hata malighafi zinazopaswa kutumika katika shughuli ya ujenzi zitumike zile ambazo zinapatikana karibu na eneo la ujenzi unapofanyika kama vile mchanga, hapa kwangu tokea ujenzi huu uanze kutekelezwa mchanga umekuwa ukichukuliwa mbali katika maeneo ya kata ya Mkako na Maguu licha ya hapa katika kata hii kupatikana mchanga mwingi unaofaa kufanyia kazi hii”, alisema Ndunguru.

Pia alisema kuwa anashangazwa na hata hivi sasa kituo hicho cha afya hakina msimamizi yaani wataalamu wa ujenzi ambao wangeweza kushauri na kusimamia shughuli za ujenzi zinazoendelea hapo badala yake wameachwa mafundi peke yao wakifanya kazi bila usimamizi wa karibu.

Aliongeza kuwa Mkurugenzi huyo wa mji wa Mbinga, Mageni ndiye aliyewafukuza wataalamu ambao ni Wahandisi wasaidizi waliokuwa hapo awali wakisimamia ujenzi huo na kwamba kuwafukuza huko alidai kuwa kunatokana na maslahi yake binafsi aliyonayo ya kutaka aweze kupata mwanya wa kufanya ubadhirifu wa fedha za mradi huo.

“Hata bati za kuezekea majengo ya kituo hiki cha afya zimekuwa pungufu baadhi ya majengo hayajaezekwa, usakafiaji wa majengo haujafanyika vifaa vya ujenzi kama vile saruji vimekuwa vikiletwa hapa kwa kusuasua ndiyo maana hata spidi ya ujenzi hakuna”, alisema.

Nao baadhi ya wananchi wa kata ya Kihungu wakizungumza kwa nyakati tofauti walidai kuwa kukwama kwa mradi huo kutokamilika kwa wakati ni kiburi alichonacho Mkurugenzi huyo ambacho kinadhihirisha wazi kuwa hata aliyekuwa Naibu Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dokta Khamis Kigwangala aliyetembelea kituo hicho mapema Julai 15 mwaka jana na kumtaka Mkurugenzi huyo kutekeleza agizo la ukarabati wa majengo yaliyopo hapo awali ya kituo cha afya Kalembo, ujenzi wa jengo la maabara na upasuaji katika eneo hilo la kituo lakini mpaka leo hii hakuna kilichofanyika licha ya Waziri huyo kutoa miezi mitatu kazi hiyo iwe imekamilika.

Walidai kuwa Serikali kuendelea kumfumbia macho mtumishi kama huyu ambaye hatekelezi kwa wakati maagizo na maelekezo yanayotolewa na viongozi wake wa ngazi ya juu ni sawa na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, Mageni alipohojiwa juu ya hali hiyo alikataa kutolea ufafanuzi tuhuma hizo huku akimjibu jeuri mwandishi wetu licha ya mwandishi huyo kwenda Ofisini kwake kutaka ufafanuzi zaidi.

Hata hivyo Serikali kwa ujumla ilitoa fedha zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu halmashauri ya mji wa Mbinga kwa ajili ya kufanya kazi ya kukamilisha ujenzi wa jengo la upasuaji, maabara, wodi ya akina mama na watoto, nyumba ya mganga pamoja na jengo la kuhifadhia maiti ambapo mpaka sasa ujenzi wake bado haujakamilika.

No comments: