Monday, January 8, 2018

OFISA KILIMO HALMASHAURI WILAYA YA SONGEA AONJA JOTO YA JIWE WAZIRI MKUU ACHUKIZWA NA UTENDAJI WAKE WA KAZI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikabidhi miche ya kahawa kwa Mkulima wa kijiji cha Lipokela Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Joseph Ngatunga inayozalishwa katika shamba la Mwekezaji mkubwa wa zao hilo Kampuni ya AVIV Tanzania Limited, hata hivyo Waziri Mkuu alichukizwa na idara ya kilimo Wilayani humo kwa kushindwa kuhamasisha wananchi kwenda kuchukua miche hiyo inayogawiwa bure na Kampuni hiyo ili waweze kupanda katika mashamba yao.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikabidhi miche ya kahawa kwa Mkulima wa kijiji cha Lipokela Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Joseph Ngatunga inayozalishwa katika shamba la Mwekezaji mkubwa wa zao hilo Kampuni ya AVIV Tanzania Limited, hata hivyo Waziri Mkuu alichukizwa na idara ya kilimo Wilayani humo kwa kushindwa kuhamasisha wananchi kwenda kuchukua miche hiyo inayogawiwa bure na Kampuni hiyo ili waweze kupanda katika mashamba yao.
Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemjia juu Ofisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea vijijini Mkoani Ruvuma, Helen Shemzigwa kwa kutosimamia ipasavyo kilimo cha zao la kahawa huku akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Saimon Bulenganija ahakikishe kwamba anawasimamia maofisa hao kwa umakini mkubwa katika Wilaya hiyo ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa mujibu wa taratibu husika.

Akizungumza na wananchi na wafanyakazi wa Kampuni ya Aviv ambayo imewekeza katika uzalishaji wa zao la kahawa katika kijiji cha Lipokela wilayani humo, mara baada ya kutembelea shamba hilo alisema jukumu la maofisa kilimo ni kuhakikisha kwamba wanakwenda kwa wakulima vijijini na kuwapa elimu ya namna bora ya uzalishaji wa mazao mbalimbali na sio muda mwingi kurundikana maofisini.

“Halmashauri ya Songea vijijini mmesema ina watumishi saba ambao wanakaa ofisini naomba kuanzia sasa Mkurugenzi uhakikishe ofisini wanaobaki ni watatu tu na wengine waende kwa wakulima", alisema.


Majaliwa alisikitishwa na uwepo kwa taarifa kuwa mwekezaji wa shamba hilo la kahawa amekuwa akitoa miche bure kwa wakulima lakini mwamko umekuwa mdogo wa wakulima, kuchangamkia miche hiyo jambo ambalo kimsingi wakwamishaji ni wataalamu wa kilimo ambao badala ya kwenda kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa upandaji wa kahawa, hupoteza muda mwingi kukaa maofisini.

Alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya AVIV, Medu Medap kwa uamuzi wao wa kugawa miche bure kwa wakulima na kwamba wakati umefika sasa kwa wakulima hao kuhakikisha kwamba wanachangamkia fursa hiyo muhimu, ambayo mwisho wa siku itawafanya wazalishe kahawa nyingi na hivyo wataweza kujikwamua kiuchumi.

“Aviv wamesema wanayo miche laki nane ambayo wanagawa bure kwa wakulima lakini hawachangamkii, sasa nakuagiza Mkurugenzi wa Songea vijijini hakikisha miche hiyo inakwenda kwa wakulima na wasimamiwe na wataalamu wako ili ipandwe haraka", alisisitiza Waziri Mkuu, Majaliwa.

Majaliwa alisema kuwa moja kati ya msisitizo wa Serikali ya awamu ya tano ni kuwataka wakulima wake wazalishe mazao yenye tija, jambo ambalo litapelekea wajikwamue kiuchumi na kuliingizia taifa fedha za kigeni na kwamba mkakati uliopo ni kuhakikisha mazao matano ya korosho, kahawa, tumbaku, pamba na chai uzalishaji wake unaongezeka.

Alisema kuwa kwa miaka ya hivi karibuni kasi ya uzalishaji wa mazao hayo umeshuka kutokana na kutokuwepo kwa mipango mizuri jambo ambalo linasababisha wakulima kugeuza mazao ya chakula kuwa ya kibiashara.

“Serikali imeamua kwa dhati kuweka nguvu kubwa katika mazao hayo ya biashara, kwani uzalishaji wake umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka na matunda yameanza kuonekana kwenye zao la korosho, kinachotakiwa hapa ni kwa wakulima kusimamiwa kwa ukaribu ili wazalishe kwa ubora", alisema.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa ameziagiza halmashauri zote nchini zihakikishe wakulima wanauza mazao yao kupitia vyama vya ushirika, kwani mfumo huo utasaidia wakulima kunufaika kwa kupata bei nzuri kwani watakuwa wakiuza wao wenyewe moja kwa moja mnadani.

Majaliwa alisema wapo wafanyabishara ambao wamekuwa wakipita kwa wakulima vijijini, na kuwarubuni wawauzie mazao yao kwa bei ya chini ambapo hilo limekuwa kikwazo kikubwa kwa wazalishaji wa kahawa na mazao mengine ya biashara kutokana na kutopata manufaa kwani hao ambao wamekuwa wakinunua kwa bei hiyo ya chini ndio wamekuwa wanufaika.

"Haiwezekani mkulima ambaye ndiye mvuja jasho shambani mazao yake yawanufaishe wale ambao wamekuwa wakikaa tu kusubiri kuwaibia, nataka halmashauri simamieni hilo tena kwa umakini mkubwa", alisema.

Alisema kuwa vitendo hivyo viovu ambavyo vimekuwa vikifanywa na wafanyabishara vimekuwa vikiwafanya wakulima wazalishe kahawa isiyo na ubora kwani kutokana na kupata bei ndogo wanashindwa kununua pembejeo za kilimo ikiwemo dawa za kuua wadudu mashambani.

Waziri Mkuu akiwa pia katika Kituo cha Utafiti wa Kahawa (TACRI) kilichopo Ugano Wilayani Mbinga Mkoani hapa alielezwa na Mkurugenzi Mkuu mtendaji wa TACRI nchini, Deusdedit Kilambo kuwa kahawa katika kituo hicho imekuwa ikizalishwa miche aina ya vikonyo ambayo haishambuliwi na wadudu kwa urahisi ambapo vikundi vya wakulima, vimekuwa vikienda kituoni hapo kufundishwa namna bora ya uzalishaji wa miche hiyo jambo ambalo limepata mafanikio makubwa.

Kwa upande wake Majaliwa alisema Serikali itaona namna bora ya kusaidia taasisi hiyo iweze kuzalisha miche kwa wingi na kusambaza kwa wakulima wake na kwamba, licha ya Serikali kuzipatia halmashauri fedha nyingi hasa kwa sekta ya kilimo wameshindwa kuzalisha miche kama TACRI inavyofanya huku akiwataka watendaji wa idara ya kilimo, kubadilika na kwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.

No comments: