Tuesday, January 16, 2018

KAMPUNI YA CHINA YASHINDA ZABUNI UJENZI BARABARA MANISPAA SONGEA KIWANGO CHA LAMI NZITO

Barabara za Manispaa ya Songea ambazo zinaendelea kujengwa.


Na Albano Midelo,        
Songea.

HATIMAYE Kampuni ya kimataifa ya China, inayofahamika kwa jina la China Sichuan International Co-operation imeshinda Zabuni ya kuendelea na ujenzi wa barabara za Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma kwa kiwango cha lami nzito.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Tina Sekambo alisema kuwa Kampuni hiyo inatarajia kuanza kazi hiyo mara baada ya kusaini mkataba baina ya Kampuni na Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Halmashauri hiyo ilivunja  Mkataba wa ujenzi wa lami nzito yenye urefu wa kilometa 8.6 kati yake na Kampuni ya Lukolo yenye makao makuu yake Jijini Dar es salaam, baada ya Kampuni hiyo kukiuka masharti ya mkataba wa miaka miwili  uliomalizika Juni 30 mwaka 2017.


Baada ya muda huo kumalizika Mkandarasi huyo aliingizwa kwenye tozo (Liquidated Damage) kwa siku 100 ambapo Oktoba 8 mwaka jana ndiyo siku 100 alizopewa Mkandarasi huyo zilimalizika hivyo Manispaa ilivunja mkataba rasmi na Kampuni ya Lukolo.

Kadhalika baada ya kuvunjwa mkataba huo, Manispaa ya Songea ilianza mchakato wa kumtafuta Mkandarasi mwingine ambapo amepatikana Mkandarasi wa Kampuni ya China Sichuan International ambaye ataendeleza kazi ya ujenzi wa barabara na kwamba, Manispaa haijapata hasara yeyote baada ya kuvunjwa kwa mkataba wa Mkandarasi wa kwanza.

Fedha za mradi huo ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 14 zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo Serikali za mitaa (ULGSP) ambapo mpango huo unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania Bara ikiwemo ya Songea.

Mradi huo ambao ulianza Juni Mosi mwaka 2015 ulitarajiwa kukamilika Juni 30 mwaka jana na kwamba barabara za Manispaa hiyo ambazo zipo kwenye mradi huu ni FFU hadi Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2, barabara ya Songea Girl’s hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5 na barabara ya Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.

Barabara nyingine ni Mitumbani hadi Yapenda yenye urefu wa kilometa moja, barabara ya Polisi hadi Stendi ya Mlilayoyo yenye urefu wa kilometa 0.45.

No comments: