Tuesday, January 23, 2018

CHANJO SARATANI KUTOLEWA BURE JAMII YATAKIWA KUPAMBANA NA UGONJWA HUO




Na Mwandishi wetu,

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kwamba kuanzia mwezi Aprili mwaka huu itaanza kutoa bure chanjo dhidi ya kirusi kinachosababisha saratani ya mlango wa kizazi (Human Papillon Virus) kwa wasichana kuanzia umri wa miaka 14.

Aidha hatua hiyo inatokana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2012 kuonyesha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na  wagonjwa wapya wa saratani ya mlango wa kizazi 51 kwa kila wanawake 100,000 huku vifo vikiwa 38 kwa kila wanawake 100,000, ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki. 

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dokta Faustine Ndugulile alisema hayo jana alipokuwa akizindua kampeni ya uchunguzi wa mabadiliko ya awali ya saratani hiyo na ya matiti, uliofanyika katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma.


Alisema hatua hiyo ya chanjo inalenga kukinga kirusi kinachoeneza saratani ya mlango wa kizazi ambayo Tanzania inaongoza kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na wagonjwa wengi.

Vilevile alisema kuwa katika awamu ya kwanza ya utoaji wa chanjo hiyo mwaka huu wamepanga kuwafikia wasichana wa kuanzia miaka 14 wapatao 616,734.

“Hawa 616,734 ndio tumepanga kuwapatia chanjo mwaka huu na katika mwaka ujao tutawafikia wasichana wa kuanzia miaka tisa hadi 14 na mwaka utakaofuata tutawapa chanjo wale wenye umri wa kuanzia miaka tisa”, alisema Dokta Ndugulile. 

Alifafanua kuwa chanjo hiyo itasaidia kuwalinda wasichana ambao wako katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa virusi vinavyosababisha saratani ya matiti na mlango wa kizazi. 

"Saratani ya mlango wa kizazi moja ya sababu ambazo zinachangia ni wasichana kushiriki ngono katika umri mdogo, kuwa na wenza wengi lakini pia kubeba mimba nyingi kunaweza kusababisha mtu kupata maambukizi”, alisema.

Aliwataka akinamama kupima afya zao mara kwa mara na wanapobainika kuwa na maambukizi, wanatakiwa kuwaona wataalamu ili kupatiwa matibabu. 

Alieleza kuwa saratani hii inatibika kabisa kama mtu atapata vipimo vya afya yake kila mara, lakini watu wengi wamekuwa wakija katika hospitali wakiwa wamechelewa hali ambayo saratani inakuwa imesambaa katika maeneo mengine ya mwili kama vile mifupa, ini na damu na kuwa vigumu kutibika.

Dokta Ndugulile aliwaagiza Wakuu wa mikoa yote hapa nchini kuhakikisha kuwa wanasimamia upimaji wa saratani ya mlango wa kizazi katika mikoa yao ili kuweza kufikia malengo ya Serikali ilivyojipangia hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu iwe imefikia akinamama milioni tatu.

Aliongeza kuwa pamoja na juhudi hizo pia Serikali hivi sasa inaboresha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ambayo ni taasisi pekee nchini katika kukabiliana na tatizo la saratani, kwa kuweka vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia kutoa huduma za matibabu ambazo zilikuwa zinatolewa nje ya nchi.

Katika mwaka 2016 Taasisi hiyo ilipokea wanawake 1,934 wa saratani ya mlango wa kizazi huku takwimu hizo zikizidi kuongezeka na kwamba jamii inapaswa kuhamasika namna ya kupambana na ugonjwa huo.

No comments: