Tuesday, January 23, 2018

SHIRIKA LA UMEME TANESCO MKOANI RUVUMA LABEBESHWA LAWAMA MADABA


Na Muhidin Amri,       
Madaba.

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoani Ruvuma, limeagizwa kufanya jitihada ya kupeleka nishati hiyo haraka katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani humo, ili watumishi waliopo huko waweze kutekeleza majukumu yao ya kutoa huduma bora kwa wananchi ipasavyo.

Aidha imeelezwa kuwa umeme huo utasaidia kupunguza gharama kubwa ya uendeshaji wa Ofisi kutokana na kutumia mafuta mengi kwa ajili ya kuendeshea Jenereta pale watumishi hao wanapofanya kazi husika.

Palolet Mgema ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songea alitoa agizo hilo juzi ambapo alisema kuwa anataka kuona TANESCO wanapeleka umeme haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo isiendelee kuwepo.


Umeme huo alisema kuwa endapo ukifika huko utaweza kurahisisha hata utendaji kazi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.

Mgema alitoa kauli hiyo baada ya baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Shafi Mpenda kwamba hadi sasa hawana huduma hiyo licha ya umeme kuanza kuwaka tangu mwezi Desemba mwaka jana.

Mpenda alisema jambo hilo limekuwa likichangia baadhi ya kazi kukwama ikiwemo hata kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki (EFDS) kwa ajili ya kukusanyia mapato ya Serikali.

Alisema kuwa TANESCO ndiyo wamekuwa kikwazo na tatizo kubwa kutokana na kushindwa kupeleka umeme katika Ofisi za halmashauri hiyo licha ya kutoa taarifa ya kuomba kuunganishiwa nishati hiyo muda mrefu uliopita.

“Tukipata nishati hii itatusaidia kupunguza gharama ya matumizi ya mafuta kwa ajili ya kuendesha Jenereta ambalo limekuwa likitugharimu fedha nyingi pale tunapotaka kutumia vifaa vya umeme”, alisema Mpenda.

No comments: