Tuesday, January 23, 2018

RAIS DOKTA MAGUFULI AMTUMBUA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA BUTIAMA



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli leo Januari 23 mwaka huu ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Butiama Mkoani Mara, Solomon Ngiliule kutokana na ubadhirifu wa fedha za umma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo ametangaza maamuzi hayo leo ikiwa zimepita siku tatu toka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotoa maagizo kwa Kaimu Katibu tawala wa Mkoa huo, Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kwenda kufanya ukaguzi maalum katika Ofisi ya Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.


Waziri Mkuu, Majaliwa aliagiza kiongozi huyo kuchunguzwa kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali ikiwemo shilingi milioni 12 walizotumia kuandaa “Profile” ya Halmashauri hiyo huku fedha zingine ni pamoja na shilingi milioni 70 za elimu maalum na milioni 288 za mradi wa maji Butiama ambazo zote hazijulikani zimetumikaje.


No comments: