Thursday, January 25, 2018

DC TUNDURU APIGA MARUFUKU WATENDAJI WA SERIKALI KUCHANGISHA WANAFUNZI MICHANGO MBALIMBALI

Na Muhidin Amri,         
Tunduru.

MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Juma Homera amepiga marufuku Walimu wa shule za Msingi na Sekondari Wilayani humo kuendelea kuwachangisha Wazazi michango mbalimbali kupitia wanafunzi wanaosoma katika shule za Serikali.

Aidha Homera amewaonya Walimu hao kwamba watakaobainika kuendelea na utaratibu wa michango hiyo, watachukuliwa hatua kali ikiwemo muhusika kufukuzwa kazi kuanzia Mkuu wa shule na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika.

Hayo yalisemwa na Mkuu huyo wa Wilaya wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa tarafa, Wakuu wa shule za Sekondari, Waratibu elimu kata, Watendaji kata na Watendaji wa vijiji katika ukumbi wa Klasta ya Walimu tarafa ya Mlingoti mjini hapa.


Alisema kuwa hapo awali kulikuwa na michango ya Madawati, chakula, michango ya Walinzi na mingine mingi ambayo ilionekana kuwa kero kwa wananchi.

Alieleza kuwa endapo Wazazi au walezi wa wanafunzi hao watakubaliana wenyewe kuchangisha baadhi ya mchango katika shule zao, Walimu wasijihusishe na chochote katika upatikanaji wa michango hiyo ili kuepuka kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya Wakuu wa shule za Sekondari za kata walisema kuwa michango ya chakula iliyokuwa ikitozwa ilitokana na makubaliano ya Wazazi wenyewe wenye watoto wao wanaosoma shuleni ambao wanaishi mbali na makazi yao.

Walimu hao walionesha mashaka kuwa utaratibu huo huenda ukasababisha utoro wa rejareja kwa wanafunzi na hivyo kushusha kiwango cha ufaulu katika vipindi vya masomo kwa watoto darasani kwa sababu hawatakuwa tayari kusoma na njaa.

No comments: