Saturday, January 6, 2018

TIMU YA UKAGUZI YAUNDWA KUCHUNGUZA UJENZI KITUO CHA AFYA KALEMBO

Ngoma mbalimbali za asili zikitoa burudani wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipowasili kwenye uwanja wa michezo Mbinga mjini.

Wananchi wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe mbalimbali wa malalamiko ambapo baadaye Waziri Mkuu aliweza kuyatafutia ufumbuzi.
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

KUFUATIA Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma kutotekeleza kwa wakati uliopangwa juu ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha afya Kalembo, kilichopo katika kata ya Kihungu ndani ya halmashauri hiyo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa tayari Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Seleman Jafo ameunda timu ya ukaguzi kwa ajili ya kwenda kuchunguza mwenendo mzima wa ujenzi wa kituo hicho.

"Ofisi yangu inazotaarifa za kutosha juu ya mwenendo wa kusuasua kwa ujenzi huu lengo tunataka tupate thamani ya matumizi ya fedha iliyotumika, nataka tumikieni wananchi hawa kwa weledi na uaminifu ili mwisho wa siku tuweze kufanya kazi yenye bora kwa manufaa ya umma", alisisitiza.

Waziri Mkuu Majaliwa alibainisha hayo jana wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.


Alisema kuwa migogoro inayoendelea katika halmashauri hiyo ndiyo ambayo inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi ikiwemo kukwamisha utekelezaji wa miradi husika.

Alimtaka Mkurugenzi mtendaji wa Mji huo, Mageni, Watumishi na Madiwani kwa umoja wao kujenga ushirikiano ili waweze kufikia malengo ya utekelezaji husika ambayo Serikali imekwisha wapatia miongozo yake namna ya kukamilisha miradi hiyo.

Kadhalika alisema kuwa ni lazima waheshimu fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi zinazotolewa na Serikali ili kuweza kufikia malengo na matakwa husika.

"Kwa mtumishi yeyote nitakayembaini amefanya ubadhirifu kwenye miradi hii ya wananchi ambayo Serikali inatumia fedha nyingi, amejenga mradi chini ya kiwango ajiandae na kufunga virago vyake atafute kwa kwenda", alisema.

Alisisitiza kuwa wale wote ambao walihusika kukwamisha mradi huo wataipata habari yao, ili iweze kuwa fundisho kwa wengine ambao hawasimamii ipasavyo miradi inayofadhiliwa na Serikali kwa manufaa ya umma.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa mji wa Mbinga, Mageni alimweleza Waziri Mkuu, Majaliwa kuwa kuanzia sasa ndani ya siku tano atakuwa tayari amekamilisha ujenzi wa mradi huo.

Pamoja na mambo mengine, Serikali kwa ujumla ilitoa fedha zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu halmashauri ya mji wa Mbinga kwa ajili ya kufanya kazi ya kukamilisha ujenzi wa jengo la upasuaji, maabara, wodi ya akina mama na watoto, nyumba ya mganga pamoja na jengo la kuhifadhia maiti ambapo mpaka sasa ujenzi wake bado haujakamilika.

No comments: