Tuesday, January 16, 2018

CHIKAMBO AWAPA SOMO WANAWAKE RUVUMA


Na Muhidin Amri,         
Songea.

MBUNGE wa Viti maalum Mkoa wa Ruvuma, Sikuzan Chikambo amewataka wanawake wa mkoa huo kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujiletea maendeleo katika familia zao na kuweza kuondokana na umaskini.

Aidha Chikambo amewakumbusha wanawake hao kutumia fedha wanazopata kuanzisha vikundi vya ujasiriamali na kutumia kwa ajili ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa nyumba bora za kuishi na kupeleka watoto wao shule.

Mbunge huyo alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wanachama wa Jumuiya  ya Wanawake ya Chama cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Songea  Mkoani hapa na kusisitiza kuwa wanawake hao wanao mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.


Chikambo alikuwa mjini hapa kwa ajili ya  kushiriki kampeni za kumnadi mgombea Ubunge wa jimbo la Songea mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dokta Damas Ndumbaro ambaye amechaguliwa na kushinda kwa kura nyingi.

Hata hivyo aliwataka kuongeza juhudi kwa kufanya kazi  na kujiunga katika vikundi hivyo sambamba na kutengeneza bidhaa zenye ubora ambao unakubalika katika viwango vya kimataifa ili waweze kuwa na uhakika wa kupata soko zuri la kuuza bidhaa zao.

No comments: