Saturday, January 13, 2018

RC RUVUMA AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUTEKELEZA WAJIBU WAO

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme.
Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme amewataka watumishi wa umma kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ili kwa pamoja waweze kufanikisha malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwaondolea kero wananchi wa mkoa huo.

Mndeme alitoa agizo hilo hivi karibuni wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya watumishi, wakuu wa idara, wakurugenzi wa halmashauri  za wilaya, mji na  wakuu wa wilaya za mkoa huo katika kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Songea Mkoani hapa.

Alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano kwa nia njema imeanzisha Wakala wa barabara mjini na vijijini (TARURA) ambaye amekwisha anza kazi na kuwezesha halmashauri kujikita katika usimamizi na utekelezaji wa shughuli nyingine za maendeleo.


Mndeme amewataka Wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za mitaa kutoa ushirikiano kwa waratibu wa TARURA kwenye maeneo yao kwa kuainisha maeneo yenye kipaumbele katika sekta ya barabara, ili wananchi  hasa wa vijijini wapate barabara zinazopitika muda wote wa mwaka.

Alisema kuwa Mkoa wa Ruvuma una mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 8520.90 kati ya hizo barabara kuu ni kilometa 925.10 na barabara za mkoa ni kilometa 1216.01 na barabara za halmashauri ni kilometa 6379.79.

Vilevile kwa upande wa barabara za lami alisema zipo zenye urefu wa kilometa 677.78 sawa na asilimia 8 ya mtandao wote wa barabara mkoani humo huku akiwataka viongozi kubuni mikakati ya kuongeza mtandao wa lami kwenye barabara zao.

Katika hatua nyingine, Mndeme amewahakikishia wananchi wa mkoa wa  Ruvuma kwamba Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kukamilisha na kuunganisha wilaya zote kwa barabara ya lami na mpango wa kuunganisha wilaya ya Mbinga na Nyasa umekamilika hivyo wakati wowote ule ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami utafanyika.

Alisema licha ya jitihada za Serikali kutengeneza barabara hizo lakini wapo baadhi ya wananchi wachache ambao wanadiriki kuhujumu miundombinu hiyo ikiwemo kupitisha mifugo kama vile ng’ombe, kulima kando kando ya barabara na  magari kubeba mizigo mizito zaidi ya viwango vilivyokubaliwa na mamlaka husababisha kuharibu na kung’oa alama za barabara.

Kutokana na hali hiyo Mkuu huyo wa mkoa, Mndeme amewaomba wananchi wenye mapenzi mema kwa nchi yao kutoa taarifa za uhalifu huo kwenye vyombo husika, kama  vile Wakala wa barabara (TANROAD) na Wakala wa usafirishaji na usimamizi wa nchi kavu na majini (SUMATRA) ili sheria ichukue mkondo wake na barabara zidumu kwa muda mrefu.

Alisema kuwa Watanzania wanashuhudia juhudi kubwa za Serikali yao katika kuimarisha ujenzi wa barabara hizo ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya Namtumbo-Tunduru-Mang’aka kilometa 193 za lami ambayo imekwisha kamilika.

Pamoja na mambo mengine kila mmoja anapaswa kuilinda miundombinu hiyo na kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa miradi kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza uzalishaji.

No comments: