Thursday, January 18, 2018

SERIKALI YASITISHA UUZAJI WA MALI ZA CHAMA CHA USHIRIKA KILIMANJARO WABADHIRIFU KUCHUKULIWA HATUA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Na Mwandishi wetu,             
Tarime.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kusitisha uuzwaji wa mali za Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU).

Majaliwa alitoa agizo hilo jana wakati alipokuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye uwanja wa Serengeti Wilayani Tarime Mkoani hapa.

Hatua hiyo imekuja baada ya KNCU kutangaza kuuza shamba lake kwa ajili ya kuiwezesha benki yake ya KCBL kutimiza sharti la mtaji la Benki Kuu ya Tanzania (BOT).


Benki hiyo ya KCBL inatakiwa kutimiza sharti la kuwa na mtaji kamili unaotosha wa shilingi bilioni 5 katika kipindi cha miezi sita tangu kutolewa kwa tangazo hilo.

Waziri Mkuu, Majaliwa alisema kuwa ni marufuku kuuza mali za ushirika huo hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inafanya uhakiki wa mali za vyama mbalimbali vya ushirika hapa nchini.

Alisisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha ushirika nchini na sasa inafanya uhakiki wa mali za vyama vyote vya ushirika na wale watakaobainika kuhusika na ubadhirifu watachukuliwa hatua.

Januari 4 mwaka huu BOT ilizipatia miezi sita benki tatu hapa nchini ili ziweze kuongeza kiwango cha mtaji unaohitajika, kutokana na matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji kamili wa kutosha.

Benki hizo ni Kilimanjaro Co-Operative Bank Limited, Tanzania Women Banki PLC na Tandahimba Community Bank Limited na pale zitakaposhindwa kutekeleza agizo hilo zitachukuliwa hatua ikiwemo kuzifutia leseni na kusimamisha shughuli za kibenki chini ya ufilisi, iwapo benki hizo zitashindwa kutekeleza agizo hilo hadi kufikia Juni 30, 2018.

No comments: