Monday, January 29, 2018

BREAKING NEWS: AFISA MISITU HALMASHAURI MJI WA MBINGA AFUKUZWA KAZI

Baraza la Madiwani Halmashauri Mji wa Mbinga, likiwa limeketi juzi kwenye kikao chake cha robo ya pili katika ukumbi wa Jumba la Maendeleo mjini hapa.


Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma limemfukuza kazi aliyekuwa Kaimu Afisa misitu wa Halmashauri hiyo, David Hyera kwa kile walichoeleza kuwa baada ya kupatikana na hatia ya kutosimamia na kutekeleza majukumu yake ya kazi za utumishi wa umma ipasavyo.

Akizungumza katika kikao cha Baraza hilo cha robo ya pili kilichoketi juzi mjini hapa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kipwele Ndunguru alisema kuwa hatua ya kumfukuza kazi mtumishi huyo pia inatokana na kushindwa kusimamia mapato ya fedha za mradi wa uvunaji wa msitu.

Ndunguru aliutaja msitu huo kuwa ni wa Mbambi ambao ni wa Halmashauri ya Mji huo na kwamba baada ya Hyera kushindwa kutekeleza kikamilifu majukumu aliyopewa alisababisha kutokea kwa wizi wa mbao na upotevu wa mamilioni ya fedha za mradi huo.


“Kamati ilipochunguza makosa yake ilimkuta ana hatia na kamati ilipendekeza apewe adhabu ya kufukuzwa kazi”, alisema Ndunguru.

Awali Baraza hilo lilisema kuwa kufuatia uzembe huo uliofanywa katika mradi huo wa uvunaji msitu wa Mbambi, wamepata hasara zaidi ya shilingi milioni 800.

Hata hivyo maamuzi hayo ya Baraza hilo yalifikiwa baada ya Kamati maalum iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kutoa taarifa yake ya uchunguzi katika baraza la dharula lililoketi Novemba 20 mwaka jana kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, ambapo baada ya kufanya uchunguzi huo waliweza kubaini mapungufu yaliyojitokeza katika shughuli hiyo ya uvunaji wa msitu.

No comments: