Monday, January 22, 2018

WAKALA WA MAJENGO RUVUMA LAWAMANI UJENZI WA OFISI MADABA


Na Muhidin Amri,   
Madaba.

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoani Ruvuma, ametakiwa kumaliza ujenzi wa majengo ya Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani humo kwa wakati uliopangwa, ili kuweza kuwafanya watumishi waweze kupata sehemu nzuri ya kufanya kazi zao pale wanapowahudumia wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme.

TBA wameonywa pia wasitumie muda mwingi kukaa Ofisini badala ya kufanya kazi husika.

Palolet Mgema ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songea alisema hayo juzi wakati alipokuwa amefanya ziara yake ya kushitukiza, kwa lengo la kukagua ujenzi huo.

Kadhalika Mkuu huyo wa Wilaya alisikitishwa kazi ya ujenzi ikiwa inasuasua huku kukiwa na idadi ndogo ya vibarua na mafundi.


Alisema kuwa kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba husika wa kazi hiyo ilitakiwa hivi sasa ifikie hatua ya kusimamisha nguzo, lakini kutokana na kasi ndogo ya ujenzi hali hiyo imekuwa kinyume na badala yake wamefikia hatua ya kuchimba mashimbo huku wakiwa nyuma ya mkataba kwa miezi mitano.

“Kwa kweli lazima niseme kweli hawa wenzetu wa TBA wanatuangusha, licha ya kuwa ni taasisi ya Serikali lakini utendaji wao wa kazi haujanifurahisha hata kidogo, wanatakiwa wahakikishe wanaongeza nguvu kazi katika mradi huu ili watumishi wetu waweze kupata ofisi za kuwahudumia wananchi”, alisema Mgema.

Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ambapo kati ya fedha hizo shilingi milioni 500 na shilingi milioni 600 zimetolewa mwezi Desemba mwaka jana, ambapo hata hivyo bado Wakala huyo wa majengo anaonekana kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka TBA ambaye ni msimamizi wa mradi huo, Ngwilimi Magese alikiri kuwa nyuma ya kazi huku akijitetea kwamba tatizo lililowafanya wachelewe ni kutokana na ukosefu wa maji na umeme.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda kwa upande wake alimshukuru Rais Dokta John Magufuli kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo huku akisikitishwa na kasi ndogo ya utendaji kazi wa Wakala huyo.

Alisema kuwa kwa mujibu wa mkataba wa mradi huo inatakiwa kila mwezi wakae kikao kimoja (Site meeting) lakini haifanyiki hivyo badala yake tangu walipokaa mwezi Novemba mwaka jana, hawajakaa tena na kila anapowakumbusha TBA kwa ajili ya kufanya hivyo wamekuwa wakikwepa kutekeleza jambo hilo.

No comments: