Saturday, January 27, 2018

SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI TUNDURU KULIMA KOROSHO

Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha kubangua korosho cha Korosho Afrika Limited kilicopo Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, wakimsikiliza juzi Mkuu a Wilaya hiyo, Juma Homera (hayupo pichani) alipokwenda kwa ajili ya kusikiliza kero zao mbalimbali.


Na Muhidin Amri,          
Tunduru.

MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Juma Homera ametoa agizo kwa shule zote za Msingi na Sekondari Wilayani humo kuhakikisha wanalima ekari tatu za zao la korosho ikiwa hapo baadaye wakati wa mavuno ndiyo sehemu ya chanzo kikuu cha mapato.

Aidha alisisitiza kuwa endapo watazingatia hilo shule hizo zitakuwa na uwezo wa kujipatia fedha na kujitegemea kutoa hata chakula shuleni kwa wanafunzi wao na kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.

Homera alikemea pia tabia ya baadhi ya wananchi kwenda kuchukua miche kwenye vitalu ambako imeeoteshwa na kuwauzia wengine kwa lengo la kujipatia fedha ambapo kwa atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.


Agizo hilo lilitolewa juzi wakati Mkuu huyo wa Wilaya akikagua vitalu vya miche bora ya korosho ambayo imezalishwa Halmashauri ya Wilaya kupitia vikundi 16 kati ya 18 katika kijiji cha Nakayaya, Nanyoka na Kangomba ikiwa ndiyo mkakati wa Serikali ya awamu ya tano katika kuimarisha na kuendeleza zao la korosho hapa nchini.

Wilaya ya Tunduru imezalisha miche ya korosho 662,163 ambayo wameanza kusambazwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali hatua ambayo imeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo Wilaya itakuwa na uwezo wa kuzalisha korosho tani 800,000 hadi milioni 1.

Vilevile ameagiza wakulima kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa kuhakikisha miche wanayopewa wanapeleka katika mashamba yao kwa ajili ya kupanda badala ya kuingiwa na tama ya kuuza kwa ajili ya kupata fedha.

“Ninaagiza sitaki kusikia miche hii inauzwa kwa mtu yeyote, Serikali imeanzisha utaratibu huu ili kuweza kuwasaidia wakulima wetu waweze kujikwamua kiuchumi, kwa hiyo haitakuwa jambo jema kuwakuta baadhi ya wapuuzi wachache wanatumia nafasi hiyo kukwamisha mpango huu mzuri wa Serikali ya awamu ya tano”, alisisitiza.

Homera alisema lengo la Serikali Wilayani Tunduru ni kuona katika kipindi cha miaka mitano ijayo shule zote za msingi na sekondari Wilayani humo zitoa chakula cha mchana na kuweza kumudu gharama ndogondogo zenyewe badala ya wakati wote kuitegemea Serikali ambayo ina majukumu mengi kwa wananchi wake.

Hata hivyo amewataka maafisa kilimo kutokaa maofisini badala yake wawe wanakwenda mashambani kwa wakulima kutoa elimu na kuwahamasisha juu ya umuhimu wa kilimo cha korosho ili kuweza kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo ambalo limeanza kuonekana lina mchango mkubwa kwa kukuza uchumi wa nchi.

No comments: