Thursday, January 18, 2018

SERIKALI YATENGA BILIONI 1 KUENDELEA NA KAZI YA UJENZI MRADI MKUBWA WA MAJI MJI WA MBINGA

Picha hii ikionyesha baadhi ya maeneo mbalimbali ya Mji wa Mbinga.


Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa Serikali katika mwaka huu wa fedha kupitia Wizara ya maji na umwagiliaji, imetenga jumla ya shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya kuendelea na kazi ya kutekeleza sehemu ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma.

Aidha mradi huo ni ule ambao kwa ajili ya kutekeleza uendelezaji wa vyanzo vinne vya maji, kutoka katika kijiji cha Tukuzi na ulazaji wa bomba kuu la uzalishaji maji kwa ajili ya kuweza kulisha Wakazi wanaoishi katika Mji huo.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) Patrick Ndunguru, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya hali ya utoaji wa huduma ya maji katika Mji wa Mbinga kwa Waandishi wa habari.


Alisema kuwa mradi huo ambao awali ujenzi wake ulipoanza zimetumika shilingi milioni 803,794,206.58 zimeweza kusaidia ujenzi wa mradi na umefikia asilimia 85 kukamilika.

Ndunguru alibainisha kuwa mradi huo utakapokamilika utaweza kuongeza kiasi cha maji kinachozalishwa kutoka mita za ujazo 2,100 hadi 4,500 kwa siku wakati mahitaji halisi hivi sasa ni mita za ujazo 5,248 hivyo itakuwa imepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji katika Mji huo.

Pia alisema kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018 MBIUWASA vilevile kwa kutumia mapato yake ya ndani imeweza kuendelea kutekeleza mradi wa upanuzi wa bomba za usambazaji maji kwa kata ya Mbambi iliyopo mjini hapa.

Alisema kuwa mpaka sasa katika kutekeleza hilo wameweza kulaza bomba jumla ya kilometa 3.5 huku wakifanya kazi nyingine za kubadilisha mita za maji zilizokwisha muda wake wa kutumika.

“Hadi sasa jumla ya mita za maji 360 zimebadilishwa kati ya malengo tuliyojiwekea ya kubadilisha mita 900 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa”, alisema.

Pamoja na mambo mengine Mji wa Mbinga unakadiriwa kuwa na wakazi 62,519 kati ya hao wakazi 28,822 ndiyo wanaopata huduma ya maji safi na salama sawa na asilimia 46.1.

Hivyo basi, mpaka sasa jumla ya wateja 2,505 wameunganishiwa maji kwa mfumo wa kufungiwa mita za maji na kufanya ongezeko la makusanyo ya mapato kutoka shilingi milioni 16.6 kwa mwezi liongezeke na kufikia shilingi milioni 23.8 kwa uzalishaji uleule uliokuwa ukifanyika.

No comments: