Sunday, January 14, 2018

DOKTA NDUMBARO ANYAKUA JIMBO LA SONGEA MJINI

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma kimeendelea kudhihirisha kukubalika kwake  na wananchi wa Wilaya hiyo, baada ya mgombea wake wa nafasi ya ubunge wa jimbo la Songea mjini Dokta Damas Ndumbaro, kupata ushindi wa kishindo katika kinyang’anyiro hicho.

Dokta Ndumbaro ambaye pia ni mwanasheria maarufu hapa nchini alipata kura 45,762 akifuatiwa na mgombe wa Chama cha CUF aliyepata kura 608, TADEA kura 471, Demokrasia makini kura 22, CCK 59, TLP 53, NRA 20, AFP 374, UDP 56 na Chama cha UPDP kimeambulia kura 30.

Kadhalika katika uchaguzi huo wananchi wengi hawakujitokeza kupiga kura, licha ya vituo vya kupigia kura kufunguliwa mapema majira ya saa moja kamili asubuhi lakini zoezi hilo lilifanyika kwa  kusua sua.


Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Songea mjini, Tina Sekambo alisema kuwa uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu ambapo hadi sasa, hakuna chama chochote kilicholalamikia matokeo hayo na kuwapongeza wananchi waliojitokeza kutumia nafasi hiyo kumpata kiongozi wanayempenda.

Uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Songea umefanyika ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mbunge wa zamani, Leonidas Gama ambaye alifariki dunia mwishoni mwa mwaka jana hivyo kutoa fursa kwa tume ya uchaguzi kutangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo.

No comments: