Tuesday, January 16, 2018

DED MADABA AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KWENDA KUWEKEZA MADABA


Na Muhidin Amri,           
Madaba.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza katika maeneo mbalimbali Wilayani humo, kufuatia Halmashauri hiyo kutajwa kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa nyingi zinazofaa kwa shughuli za uwekezaji hapa nchini.

Mpenda alitoa wito huo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na fursa  rafiki zilizopo huko ambazo bado hazijafanyiwa kazi licha ya Wilaya ya Madaba kutajwa kuwa ni sehemu nzuri kwa shughuli za uwekezaji.

Alisema kuwa Halmashauri hiyo bado kuna rasilimali nyingi ikiwemo ardhi nzuri yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali kama vile kahawa, chai, korosho, mahindi tangawizi pamoja na uwepo wa mto Ruhuji wenye samaki wengi wazuri ambao hawapatikani sehemu yoyote hapa nchini na misitu mikubwa yenye wanyama kwa ajili ya shughuli za utalii na uwindaji.


“Madaba inaendelea kukua siku hadi siku, hata hivyo bado tunakabiliwa na changamoto ya nyumba za kulala wageni, viwanda nawaomba watu waje kuwekeza katika halmashauri hii”, alisema.

Mkurugenzi huyo aliahidi Serikali kupitia Halmashauri hiyo itaendelea kuweka mazingira bora na rafiki ya uwekezaji na wawekezaji na sasa inaendelea kuboresha huduma zote muhimu  kama vile huduma ya maji safi na salama, afya, barabara na huduma za mawasiliano.

Mpenda amewatoa hofu watu wanaohitaji kuwekeza na kuwaeleza kwamba Madaba ni mahali safi na salama kwa ajili ya kuwekeza katika miradi ya kiuchumi kama inavyosisitizwa na Serikali ya awamu ya tano  chini ya Rais Dokta John Magufuli.

Katika hatua nyingine Mpenda, amewataka watumishi wa umma kuongeza juhudi ya kazi pamoja na kutoa ushirikiano kwa watu wanaokwenda kuwekeza miradi ya kiuchumi huku akisisitiza umuhimu wa wananchi nao kutumia muda wao kwa ajili ya kufanya kazi za kujiletea maendeleo.

No comments: