Thursday, January 11, 2018

WAPONGEZA JITIHADA ZA RAIS AWAMU YA NNE KUIGAWA WILAYA YA MBINGA

Na Muhidin Amri,     
Nyasa.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amempongeza Rais wa awamu ya nne, Dokta Jakaya Kikwete kwa uamuzi wa kuigawa Wilaya ya Mbinga  iliyopo Mkoani Ruvuma na kuzaliwa Wilaya ya Nyasa Mkoani humo kwa lengo la kusogeza huduma mbalimbali za kijamii karibu na wananchi.

Majaliwa alitoa pongezi hizo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi wa Wilaya Nyasa, wakati akifunga Tamasha  la utalii katika viwanja vya Bandari ya Mbamba bay wilayani hapa.

Waziri Mkuu amewataka wananchi wa Nyasa kuwa na tabia ya kuwaenzi viongozi na watumishi wanaofanya vizuri katika  kuwaletea maendeleo, ili kuepusha kuwakatisha tamaa jambo linaloweza kurudisha nyuma dhamira ya kimaendeleo waliyonayo viongozi hao.


Aidha Majaliwa aliwajia juu baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hata wa vyama vingine ambao wameanza kujipitisha pitisha katika jimbo la Nyasa  kwa lengo la kuwashawishi wananchi ili waweze kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Alisema kuwa Wabunge wote wa mkoa wa Ruvuma wako imara katika kutekeleza majukumu yao  kwa wananchi, kwa hiyo hawahitaji kuanza kubugudhiwa na wajanja wachache ambao wameanza kujipitisha kwa lengo la kutaka kugombea.

Katika hatua nyingine Waziri mkuu huyo amewataka watumishi wa umma katika wilaya hizo kuacha urasimu kwa kutoa huduma kwa upendeleo na wengine kutoa kwa kujuana badala  yake watoe huduma  kama ilivyoagizwa na Serikali ya awamu ya tano. 

Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwatumikia wananchi, hivyo watumishi wa umma ni lazima watambue kuwa jukumu lao ni kumaliza kero za Watanzania badala ya kujifanya Miungu watu tabia ambayo inachangia kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

No comments: