Saturday, January 6, 2018

SERIKALI IMEFUTA KUTOLEWA KWA VIBALI KWA MAKAMPUNI BINAFSI KUNUNUA ZAO LA KAHAWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza Madiwani na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga katika ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa. 
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefuta vibali kwa makampuni binafsi yanayonunua zao la kahawa hapa nchini na kuwataka viongozi husika kutekeleza agizo hilo bila kuchelewa.

Majaliwa alisisitiza kuwa kuanzia sasa biashara yote ya zao la kahawa itafanywa na vyama vya ushirika vilivyosajiliwa na kutambuliwa kisheria na sio vinginevyo.

"Tunataka turekebishe ushirika mkuu wa wakulima wa kahawa MBIFACU uliopo hapa wilayani Mbinga, ili uweze kuwasaidia wakulima hawa na hatimaye wajikwamue na umaskini", alisema.


Waziri Mkuu, Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mbinga katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo uliopo mjini hapa.

Alibainisha kuwa vibali vya ununuzi wa kahawa ambavyo vinatolewa na halmashauri za wilaya kwa makampuni binafsi ndiyo chanzo kinachosababisha mkulima apate hasara na kuendelea kuwa maskini.

Ameyataka makampuni yote yaliyokuwa yakifanya biashara ya kununua kahawa yaende yakafanye biashara hiyo mnadani na kwa wale watakaopuuza agizo hilo wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria. 

Vilevile alimtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo kuhakikisha kwamba anasimamia kikamilifu maagizo yanayotolewa na Serikali ili wakulima wasiweze kupata hasara.

Majaliwa aliongeza kuwa hataki kusikia biashara ya Magoma ya kahawa inaendelea kufanyika na yule ambaye atabainika kuhusika na biashara hiyo akamatwe na kufikishwa Mahakamani.

"Mtu wa namna hii mkisha mbaini huyo ni mwizi tena ni mhujumu wa uchumi, Magoma ndiyo yanayowaibia fedha wakulima kwenye mazao yao huu ndiyo msimamo wa Serikali Mkuu wa wilaya na viongozi wenzako simamieni hili", alisisitiza Majaliwa.

No comments: