Wednesday, January 17, 2018

JUHUDI LITUMBANDYOSI MBINGA KUANZISHA DUKA LA PEMBEJEO ZA KILIMO CHA KOROSHO

Baadhi ya wanachama wa kikundi cha Juhudi, kilichopo katika kijiji cha Litumbandyosi kata ya Litumbandyosi wakiwa kwenye kitalu cha miche bora ya mikorosho ambayo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, kwa kushirikiana na wanakikundi hao wamezalisha miche hiyo kwa ajili ya kuwagawia bure wakulima wa korosho katika kata hiyo ili waweze kuipanda kwenye mashamba yao katika msimu wa mwaka huu.


Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

WANACHAMA wa kikundi cha Juhudi waliopo katika kijiji cha Litumbandyosi kata ya Litumbandyosi Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, ambao wanajishughulisha na kilimo cha zao la korosho wanatarajia kuanzisha duka la pembejeo la zao hilo ili waweze kupata pembejeo kwa urahisi.

Mhasibu wa kikundi hicho, Athanas Nyimbo aliwaeleza Waandishi wa habari kuwa kuanzisha kwa duka hilo wanatarajia kuanza na mtaji wa shilingi milioni mbili, fedha ambazo watapewa na Serikali kutokana na mgawo wa asilimia 30 baada ya kazi waliyofanya ya uzalishaji wa miche bora ya korosho ambayo itaanza kusambazwa kwa wakulima wa kijiji hicho.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa duka hilo itakuwa ni msaada mkubwa kwao katika kijiji hicho na maeneo mengine ya jirani na kata ya Litumbandyosi, kwani hivi sasa wamekuwa wakilazimika kufuata huduma ya pembejeo za korosho umbali mrefu Wilayani Tunduru.


Serikali imedhamiria kufufua na kuendeleza zao la korosho pamoja na mazao mengine makubwa ya biashara ikiwemo Pamba, tumbaku, chai na kahawa ambapo katika Wilaya ya Mbinga zao la korosho limekuwa likistawi vizuri katika maeneo ya kata hiyo kutokana na kuwa na hali ya hewa nzuri ya joto.

Nyimbo alieleza kuwa awali pembejeo za  zao hilo pamoja na kuzifuata mbali zimekuwa zikipatikana kidogo na kwamba hazitoshelezi mahitaji halisi ya wakulima wake jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya wakulima kukata tamaa kuendelea na kilimo cha zao la korosho.

Aliongeza kuwa baada ya Serikali kuhamasisha ufufuaji wa kilimo cha zao hilo hivi sasa idadi ya wakulima imezidi kuongezeka kutoka 300 hadi kufikia wakulima 2,000 katika kijiji cha Litumbandyosi na kwamba wanatarajia idadi hiyo kuzidi kuongeza hasa katika msimu wa mwaka huu baada ya Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kuanza kuzalisha miche bora ya zao la korosho ambayo wakulima watagawiwa bure ili waweze kuipanda katika mashamba yao.

Vilevile alisisitiza kuwa hivi sasa wanaiomba Serikali kupitia wataalamu wake wa kilimo waliopo katika Halmashauri za Wilaya, wapite vijijini mara kwa mara kwa wakulima kuwaelimisha juu ya mbinu bora za kilimo cha zao hilo ikiwemo na matumizi sahihi ya pembejeo za zao la korosho.

No comments: